May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema kubadili msimamo Jimbo la Muhambwe? Mkosamali…

John Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kitaamua ndani ya saa 48, kuanzia leo Jumatatu, kama kitajitosa katika uchaguzi wa ubunge wa Muhambwe, mkoani Kigoma au la. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Chadema kimetoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 29 Machi 2021, kupitia kwa John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, alipokuwa akijibu swali la MwanaHALISI Online.

MwanaHALISI Online, lilitaka kujua kama Chadema kitashirika uchaguzi huo mdogo wa tarehe 2 Mei 2021, au la, Mrema amesema “kuna kikao kitafanyika hadi kesho, tutatoa uamuzi wa chama.”

Mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020, Chadema kilitangaza kutoshiriki uchaguzi wowote hadi pale itakapopatikana Tume Huru ya Uchaguzi.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanania, kikirejea kushiriki uchaguzi, kitakuwa kimebadili msimamo wake na mmoja wa kiongozi wa chama hicho, ameudokeza mtandao huo akisema “huu ni utawala, mwingine wa mama (Rais Samia Suluhu Hassan), hivyo, kuna uwezekano mkubwa tukashiriki.”

Kiongozi ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amesema “unajua hata unavyoona, mama alisema tusahau yaliyopita tusonge mbele, kwa maana hiyo, wacha tushiriki harafu tuone, anachokisema anakimaanisha kuwa tume hii hii inaweza kutenda haki.”

Marehemu Atashasta Nditiyea aliyekuwa Mbunge jimbo la Muhambwe

Kwa sasa Tanzania, inaongozwa na Rais Samia kuanzia tarehe 19 Machi 2021, baada ya aliyekuwa Rais, John Pombe Magufuli, kufariki dunia 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na kuzikwa Ijumaa iliyopita, nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.

Chadema ilitoa kauli hiyo ya kushiriki au la, ikitanguliwa na iliyotolewa na Felix Mkosamali, aliyegombea jimbo hilo katika uchaguzi mkuu uliopita akisema “nitafanya uamuzi leo au kesho.”

Alipoulizwa msimamo wa chama chake katika hilo ni upi, Mkosamali amesema “nafikiri nao leo au kesho, watakuwa wamefanya uamuzi, lakini huwa niko imara na wao wenyewe CCM wanafahamu kuwa hakuna lelemama.”

Mkosamali aliongoza jimbo hilo kati ya mwaka 2010-2015 akiwa NCCR-Mageuzi na uchaguzi mkuu wa 2015, alishindwa na Nditiye na hata uchaguzi mkuu wa 2020, akiwa Chadema akashindwa tena na Nditiye.

Ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuhusu uchaguzi huo, inaonyesha shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu imeanza jana Jumapili 28 Machi hadi 3 Aprili, 2021.

Uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hiyo ukifanyika tarehe 3 Aprili 2021.Kampeni za uchaguzi katika jimbo hilo zitaanza 3 Aprili 2021 hadi 1 Mei na siku inayofuata ambayo ni 2 Mei 2021, ni siku ya uchaguzi huo.

error: Content is protected !!