MWENYEKITI wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe anatarajiwa kuongozi jopo la viongozi wa chama hicho katika uzinduzi rasmi wa mikutano ya hadhara itakayofanyika jijini Mwanza tarehe 21 Januari, kisha tarehe 22 wilayani Musoma katika Kanda ya Serengeti.
Mbowe anatarajiwa kuambatana na viongozi wengine wa ngazi ya taifa akiwepo Katibu Mkuu wa Chama, John Mnyika na Manaibu Katibu Wakuu. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 15 Januari, 2023, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Itikadi na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Kamati kuu ya Chama hicho iliyoketi tarehe 5 Januari, mwaka 2023 kwa njia ya mtandao, kuazimia uzinduzi wa mikutano ya hadhara ifanyike tarehe 21 mwezi huu.
Amesema wanazindua mkutano tarehe 21 Januari, 2023 kwa sababu ni siku kubwa kwa chama hicho.
“Ni siku yenye historia kubwa, ni tarehe ambayo chama chetu kilipata usajili wa kudumu tarehe 21 Januari, 1993. Chama chetu kinakwenda kutimiza miaka 30 tangu tumepata usajili wa kudumu. Kwa hiyo tunapokwenda kuzindua mikutano ya hadhara tarehe hiyo, Chama kinakwenda kutimia miaka 30 tangu kilipopata ya usajili wa kudumu.
“Ni tarehe ambayo ina historia na chama chetu, ndio maana tukaichagua kwamba baada ya miaka saba ya kutoruhusiwa kufanya siasa za jukwaani, tukafanye uzinduzi wa tarehe hiyo,” amesema.
Amesema uzinduzi huo utaambatana pia na ajenda za kitaifa za mikutano ya hadhara kwani kuna mambo ambayo watakwenda kuyasema na ndio yatakayowaongoza katika mikutano yote ya hadhara na baada ya uzinduzi huo ngazi nyingine zitaendelea.
Ameongeza kuwa maandalizi yameshaanza na yanaendelea kwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika pamoja na kulipia viwanja kesho Jumatatu kwa sababu kuna viwanja vinamilikiwa na halmashauri.
“Tumejulishwa kwamba tangu wiki iliyopita hakuna mtu mwingine aliyeviomba. Tutapelekwa taarifa rasmi kwenye mamlaka husika ikiwamo utaratibu wa kupatiwa ulinzi, hatutegemei kwamba kutakuwa na figisu zozote sasa,” amesema.
Leave a comment