August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema kuahirisha tena Ukuta?

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

KESHO Ijumaa ya tarehe 30 Septemba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huenda kikatangaza kuahirisha tena uzinduzi wa operesheni iliyobatizwa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), anaandika Charles William.

Uzinduzi wa operesheni Ukuta, ulitangazwa tarehe 27 Julai mwaka huu na kwamba ungefanyika mnamo Septemba Mosi, mwaka huu hata hivyo uliahirishwa siku moja kabla ya kufanyika kwake kutokana na kile kilichoitwa, ‘ombi la viongozi wa dini’.

“Tunatangaza kuahirisha mikutano na maandamano ya Ukuta kwa kuwa viongozi wa dini, wametuomba tuwape angalau wiki tatu ili wafanye mazungumzo na Rais John Magufuli ili kutafuta suluhu ya suala hili na kama ikishindikana basi tutaifanya Oktoba mosi mwaka huu,” alisema Freeman Mbowe Agosti 31, mwaka huu.

Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni.

Hata hivyo, wiki iliyopita Salum Mwalimu, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, alipoulizwa na MwanaHALISI Online kuhusu uzinduzi wa operesheni hiyo hasa ikizingatiwa kuwa zimebaki siku chache kabla ya Oktoba Mosi, alijibu kuwa, “Ukuta siyo tarehe.”

“Ukuta ni fikra zinazoishi ndani ya mioyo ya watu na zitaendelea kuishi. Suala siyo kubaki kwa siku tano au kumi. Tunasubiri tupate mrejesho kutoka kwa viongozi wa dini halafu tutafanya uamuzi juu ya suala hilo,” alisema.

Tumaini Makene, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, ametoa taarifa jioni ya leo akisema, chama hicho kitatoa tamko juu ya suala hilo siku ya kesho.

“Taarifa rasmi kuhusu Ukuta na hatima ya siku ya maandamano na mikutano nchi nzima iliyotangazwa na chama, itatolewa kesho Ijumaa, Septemba 30, 2016, saa 5:00 asubuhi, mzungumzaji mkuu atakuwa ni Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama Taifa,” amesema Makene.

Dalili za awali zinaonyesha kuwa, Chadema inaweza kuahirisha tena kufanyika kwa uzinduzi wa operesheni hiyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuchelewa kupata majibu ya viongozi wa dini juu ya jaribio lao la kuonana na Rais John Magufuli ili kutafuta suluhu.

Taarifa zaidi zinadai kuwa, mpaka sasa jaribio la viongozi wa dini kuonana na Rais Magufuli na kujadili suala la kuruhusu kufanyika kwa mikutano na maandamano nchi nzima limegonga mwamba.

Pia chama hicho kinaonekana kutofanya maandalizi yoyote ya msingi kulinganisha na joto la maandalizi lililokuwepo kuelekea uzinduzi wa operesheni hiyo Septemba Mosi mwaka huu kabla ya kuahirisha.

Itakumbukwa kuwa, wiki mbili zilizopita, gazeti moja la kila siku liliripoti kuwa Rais Magufuli amekataa kuonana na viongozi wa dini ili kuzungumzia suala la Ukuta.

Habari ya gazeti hilo ilikuwa na kichwa cha habari, “Rais Magufuli awatosa viongozi wa dini.”

Vuguvugu la uzinduzi wa operesheni Ukuta mwezi uliopita, lilisababisha jumla ya wanachama na viongozi wa Chadema 230 kukamatwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na wengine 28 kushikiliwa mahabusu mpaka tarehe 1 Septemba ilipopita.

error: Content is protected !!