Sunday , 25 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema kinakwenda Buyungu kushiriki uchaguzi au kushinda?
Habari za SiasaTangulizi

Chadema kinakwenda Buyungu kushiriki uchaguzi au kushinda?

Spread the love

KIPYENGA cha kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Buyungu, wilayani Kakoko, mkoani Kigoma, kimepulizwa. Anaripoti Yusuph Katimba … (endelea).

Uchaguzi mdogo wa Buyungu unafanyika kufuatia kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wa Chadema, katika jimbo hilo, Mwalimu Samson Kasuku Bilago.

Mwalimu Bilago (54), alifikwa na mauti katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu, terehe 26 Mei mwaka huu.

Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kuota kinyama sehemu ya haja kubwa unaofahamika kwa jina la hemorrhoids au piles – (bawasiri).

Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC), imetangaza kuwa uchaguzi huo utafanyika tarehe 12 Agosti. Tayari kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa Buyungu, zimeanza.

Katika uchaguzi huu, ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya wagombea wa wawili wenye nguvu – Mhandisi Christopher Chiza (CCM) na Elias Kanjero (Chadema).

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliyopita, upinzani umeshinda kiti kimoja pekee cha udiwani mkoani Mbeya.

Swali ambalo baadhi ya wananchi wanajiuliza ni hili: Je, Chadema kinakwenda Buyungu kushiriki uchaguzi au kinakwenda kushinda?

Kama kinakwenda kushinda, iko wapi mikakati, mbinu na maarifa ya kufikia ushindi huo? Wako wapi wapiganaji wa kukabiliana na “maharamia” ya CCM?

Hakuna shaka kuwa iwapo Chadema kingeweka nguvu zinazostahili Buyungu, kingeweza kushinda uchaguzi huu.

Hii ni kutokana na aina ya mgombea – Christopher Kajoro Chiza (65) – ambaye amepelekwa na chama tawala kwa wananchi, kuchafuka kwenye macho ya wapigakura.

Chiza alikuwa mmoja wa mawaziri wandamizi katika serikali ya Jakaya Kikwete na mbunge wa jimbo la Buyungu kwa zaidi ya miaka 10.

Hata hivyo, katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, aliangushwa mithili ya “gogo kavu” na Mwalimu Bilago.

Ushindi wa Bilago, pamoja na mambo mengine, ulitokana na “chuki ya wananchi dhidi ya Chiza.”

Lakini katika uchaguzi huu mdogo, hakuonekani mipango ya Chadema, hasa katika kukabiliana na hila, mizengwe, hujuma na “tekrenolojia ya uchaguzi ya CCM.”

Aidha, ndani ya Buyungu, hakuonekani mikakati ya chama hiki katika kukabiliana na ghiriba, mabavu na vishawishi vya rushwa ya fedha na madaraka vinavyotumiwa na CCM katika kujitafutia ushindi.

Wala hakuonekani utayari wa viongozi wake, kukemea viongozi wa serikali na vyombo vyake vya usalama, waliojiingiza kwenye uchaguzi, badala ya kulinda usalama wa raia.

Pamoja na wito wa mgombea wao – Elias Kanjero – kuwa marehemu Kasuku Bilago – anaangalia yanayoendelea Buyungu kupitia ulimwengu wa kiroho, hakuna kunakoonekana mikakati ya kulinda mbegu hii.

Hakuna kunakoonekana kulindwa kwa mbegu hii iliyopandwa na Bilago Buyungu, ili isikauke. Hakuna.

Bali, kinachoonekana machoni mwa wengi, ni viongozi wa chama hiki kuwa katika mchoko. Wengi wakifikiria mwaka 2020 watakavyoweza kurudi bungeni kwa “mlango wa nyuma.”

Wengine wameelekeza akili zao kwenye kutetea viti vyao ndani ya chama na kulinda maslahi yao baada ya mwaka 2020.

Aidha, kama Chadema kingetaka kushinda Buyungu, kingepaswa kuanza kuwekeza mara baada ya Mwalimu Bilago kufariki dunia.

Kingekwenda Buyungu, siyo tu kumzika Bilago, bali kutetea ambacho amekipigania na kukilinda kwa miaka zaidi ya miwili na nusu ya ubunge wake.

Tokea siku alipozikwa, Chadema kingeweka kambi Buyungu na kufanya kampeni bila kuchoka. Kingekwenda kufanya mashambulizi dhidi ya chama tawala na viongozi wake, jambo ambalo lingesababisha kurudisha nyuma mikakati yao ya hujuma.

Chadema kingebaki Buyungu kueleza wananchi maovu ya chama tawala kwa lengo la kujenga chuki ya wananchi dhidi ya chama hicho.

Lakini kimeshindwa kufanya hivyo. Kimeshindwa kutambua kuwa chenyewe ndio chachu ya ushawishi wa vyombo vya habari hapa nchini.

Hili na mengine ambayo yalikuwa yanaonekana kuwa na afya kwa chama, yameshindikana kwa sababu, viongozi na wanachama wa chama hiki, wamekosa umoja na upendo wa kweli, na kwamba pale wanapokosana wanaona kuwa njia pekee ya kurekebishana ni kutuhumiana.

Sababu nyingine inayochangia kudhoofisha Chadema, ni viongozi wake kufanya kampeni za kizamani wakati dunia inabadilika. Ndani ya chama wamekosekana viongozi mahili wa kampeni, hasa watu wanaoheshimika ndani na nje ya chama.

Baadhi ya watu hawapaswi kuzungumza na vyombo vya Habari kwa niaba ya chama. Ni kutokana na kuwa miongoni mwa watu ambao hawana heshima kubwa kiasi hicho katika jamii.

Yawezekana wapo watakaosema, nilichoandika na kukijadili, siyo sahihi. Lakini ni vema tukasubiri, muda ndio utakaoamua.

Mwandishi wa makala hii, Yusuph Katimba, ni mhariri wa gazeti la kila wiki la SMATI. Anapatikana kwa simu Na. 0782 001689.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

Habari MchanganyikoTangulizi

25 wafariki dunia katika ajali Arusha

Spread the loveWatu 25 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Biteko afuta likizo watumishi Tanesco, bosi Morogoro yamkuta

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dk. Doto...

Habari za Siasa

Mbarala ajitosa kumrithi Zitto, aahidi kuipa ushindi ACT-Wazalendo uchaguzi mkuu

Spread the loveKATIBU wa Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalum...

error: Content is protected !!