Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema, kina mdee vitani tena
Habari za Siasa

Chadema, kina mdee vitani tena

Halima Mdee
Spread the love

 

MKAKATI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kuwang’oa bungeni, waliokuwa wanachama wake 19, wakiongozwa na Halima James Mdee, umegeuka vita ya pande hizo mbili, imebainika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Chadema wameitisha mkutano wa Baraza Kuu la Taifa (BKT), mwezi huu, Mbeya, ili pamoja na mambo mengine, kujadili rufaa ya Mdee na wenzake, wanaowatuhumu kujipeleka bungeni, kinyume na maelekezo ya chama.

Mnyukano wa sasa, unatokana na hatua ya baadhi ya viongozi wakuu wa Chadema, kujiapiza kuwa ni sharti uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya kuwafuta uanachama Mdee na wenzake, ubaki kama ulivyo, huku wenyewe wakijihami kwa gharama zozote, kuendelea kubaki bungeni na kurejeshewa uanachama wao.

Mdee ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) pamoja na wenzake, wamewasilisha rufaa Baraza Kuu, kupinga uamuzi wa Kamati Kuu, iliyokutana tarehe 27 Novemba 2020 wa kuwavua nyadhifa za uongozi na kuwafuta uanachama.

Walituhumiwa na kupatikana na hatia kwenye makosa kadhaa yakiwamo usaliti, uchonganishi, kughushi nyaraka, ubinafsi, upendeleo na kujipeleka bungeni na kujiapisha kuwa wabunge wa Chadema, kinyume cha taratibu na maelekezo ya vikao vya chama.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa CC, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa Katibu Mkuu Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo (Bara) na Hawa Bananga Mwaifunga.

Wengine, ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Katika orodha hiyo, wamo pia Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Watuhumiwa hao, waliopachikwa jina la Covid-19, wamewasilisha rufaa ya kupinga kuvuliwa uanachama wao, wakieleza “mchakato mzima wa kuwafukuza, haukufuata taratibu.”

Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, Baraza Kuu, ndicho chombo cha mwisho cha rufaa kwa wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, mameya na wenyeviti wa halmashauri.

Taarifa zinasema, Sektarieti ya Chadema, imependekeza kufanyika kwa kikao cha Kamati Kuu, muda wowote mapema wiki ijayo, kupanga maandalizi ya Baraza Kuu, litakalotoa nafasi kwa rufaa hizo kufanyiwa uamuzi wa mwisho.

Watuhumiwa wote 19, tayari wamekabidhiwa barua zao za kuwajulisha kuwapo kwa mkutano huo wa Baraza Kuu na kuelezwa kuwa watajulishwa mahali mkutano utafanyika.

“Katibu Mkuu, John Mnyika, baada ya kushauriana na Mwenyekiti, kama Katiba inavyoelekeza, atatoa taarifa ya kuwapo kikao cha Kamati Kuu na baadaye kikao cha Baraza kitafanyika, ili kumaliza shauku ya wanachama juu ya jambo hili,” alieleza mmoja wa viongozi waandamizi wa Chadema, kwa sharti la kutotajwa jina.

Taarifa kutoka ndani ya Chadema na baadhi ya watuhumiwa hao zinasema, tayari Mdee na wenzake, wamejipanga kuzuia kufukuzwa kwa kuhakikisha kikao cha kuwajadili, hakifikii maazimio yanayotarajiwa.

Miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kutekelezwa na watuhumiwa hao, ni kila mmoja kupata wajumbe wa Baraza Kuu wasiopungua 10, ambao watawaunga mkono ili kuhakikisha hawaondoki ndani ya chama hicho.

Baraza Kuu la Chadema, lina wajumbe takribani 500 na kila mmoja wa watuhumiwa atafanikiwa kupata idadi waliyokubaliana, basi karibu nusu ya wajumbe watakuwa upande wao.

“Haya ninayokueleza, ndiyo waliyokubaliana kwenye kikao chao kilichofanyika hapa Dodoma, baada ya kumalizika mkutano wa Bunge la Bajeti,” alieleza mmoja wa watu walio karibu na wabunge hao, ambaye hakupenda kutajwa jina lake

Aliongeza: “Kwamba kila mmoja atafute watu wasiopungua 10 kutoka kwenye mkoa wake na mikoa jirani, ili kuhakikisha Baraza Kuu, linafuta azimio la Kamati Kuu la kuwafuta uanachama.”

Alisema mbali na wajumbe hao wa Baraza Kuu, kundi hilo limepanga kuandaa wapambe kadhaa, watakaobeba mabango ya kushinikiza wajumbe wa kuwarejeshea uanachama wao.

Alipoulizwa wanawezaje kukabiliana na wafuasi na wanachama wa Chadema, ambao wamechukizwa na hatua ya watuhumiwa hao kwenda bungeni, kinyume na maelekezo ya chama, mtoa taarifa huyo alisema: “Siwezi kusema. Lakini wamejiandaa vya kutosha.”

Kundi hilo, limepanga kukabiliana na fujo zozote zitakazotokea, ikiwamo kuhakikishiwa ulinzi wa usalama wao, muda wote wa kikao na baada ya kikao hicho kufanyika.

“Safari hii, wamejiandaa kwenda mbele ya Baraza Kuu, kwa kuwa tayari wamehakikishiwa ulinzi wa usalama wao na mali zao. Wanawajua watu wa Chadema jinsi wanavyotawaliwa na mihemko, wamejipanga kukabiliana na kila kitu,” alieleza mmoja wa wafuasi wa wabunge hao.

Alisema: “Mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti, walikutana kupanga mkakati wa kukabiliana na Chadema na walifanya hafla pale Royal Hotel, ambayo ilihudhuriwa na wabunge wote 19 isipokuwa Makamba (Salome), ambaye alikuwa na matatizo ya familia.

“Hapo ndipo walipotangaza msimamo wa kwenda kwenye Baraza Kuu, Julai 24 na kukabiliana na kila atakayejitokeza kutaka kuwaondoa bungeni,” alisema.

Aidha, mtoa taarifa huyo anasema, ikiwa mkakati wao wa kuzuia kufukuzwa utafeli, basi mpango wao wa pili, ni kukimbilia mahakamani, ili kuomba mahakama isitambue uamuzi uliofikiwa hadi shauri watakalofungua limalizike.

Mbali na Mahakama, mtoa taarifa alisema Mdee na wenzake, wamepanga kupigania wanachoita, haki yao, kupitia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Alisema: “Hakuna ambaye yuko tayari kuomba radhi, kwa kuwa ukiomba msamaha, maana yake unapoteza ubunge, jambo ambalo miongoni mwao, hakuna aliye tayari kulitekeleza.

“Moja ya sababu kubwa ambazo zinawafanya wasikubali kupoteza ubunge, tayari wamechukua mikopo kwenye benki, ambayo itakuwa shida kurejesha.”

Hata hivyo, mtoa taarifa huyo alisema, baadhi ya wahusika, wana shaka kubwa na Nusrat, kwamba anaweza kurudi kundini, kutokana na kuonekana bado anapenda siasa za Chadema.

Alisema katika kukabiliana na halo, wamemwekea kikosi kazi cha kumlinda na kumshauri, ili kuhakikisha harudi nyuma.

Tangu Chadema iamue kuwafututa uanachama Mdee na wenzake, Spika Ndugai, amekuwa akiwakingia kifua, kwa kueleza kuwa hawezi kuwaondoa bungeni, kwa kuwa wamewasilisha rufaa Baraza Kuu na bado hawajasikilizwa.

Aidha, Spika Ndugai amenukuliwa akisema, kabla ya kuchukua hatua zozote za kumfukuza mbunge, ni sharti chama kilichofikia uamuzi huo, kiwasilishe kwake mwenendo wa uamuzi uliofanywa na vikao husika, ukiwa umeambatana na orodha ya wajumbe wa vikao na kuongeza: “Huo ndio utakuwa utaratibu wa kushughulikia masuala ya aina hiyo, kuanzia sasa.”

Alisema, baada ya kupokea nyaraka hizo, atawaita wahusika na hatafanya uamuzi wa kuondoa mbunge bungeni, bila kumpa nafasi ya kusilikizwa, jambo linalotafsiriwa na wachambuzi wa kisiasa, kuwa linalenga kumbeba Mdee na wenzake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!