Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema Karatu mbioni kupasuka  
Habari za SiasaTangulizi

Chadema Karatu mbioni kupasuka  

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

NGOME pekee ya Chama cha Demokrasia naMaendeleo (Chadema), iliyokuwa imesalia – halmashauri ya wilaya ya Karatu – iko hatarini kuvunjika muda wowote kutoka sasa. Anaripoti Aidan Aziz … (endelea). 

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho wilayani Karatu zinasema, ngome hiyo yaweza kuvunjika kufuatia kuibuka mgogoro mkubwa wa uongozi uliotokana na uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo kupitia Chadema. 

Tayari madiwani wawili wa chama hicho katika halmashauri ya Karatu, Yotham Manda, aliyekuwa diwani wa kata ya Qurus na Ally Bytoo, aliyekuwa diwani wa kata ya Endamaghan, wamejiuzulu nafasi zao.

Yotham alikuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo. Wote wawili wametangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na tayari wamefanya hivyo jana Jumapili.

Madiwani wengine wanne wa kata, taarifa zinasema, wako mbioni kuondoka ndani ya chama hicho, kabla ya Oktoba mwaka huu.

Mgogoro wa sasa ambao unahatarisha uwezo wa Chadema kuendelea kuongoza halmashauri ya wilaya ya Karatu, unatokana na kuibuka makundi mawili makubwa ya uongozi ndani ya wilaya hiyo.

Kundi la kwanza, linaongozwa na mbunge wa Viti Maalum, Cecil Pareso na jingine ni lile linalomuunga mkono mbunge wa jimbo, Willy Qambalo.

Cecil anayeungwa mkono na mwenyekiti wa halmashauri, Jubleti Mnyenye, anajipanga kimkakati kumng’oa Qambalo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, tayari mbunge huyo aliyejiapiza “liwe jua, iwe mvua,” sharti atagombea ubunge wa jimbo la Karatu katika uchaguzi ujao, ameanza kuwashughulikia watu wote wanaomuunga mkono Qambalo.

Miongoni mwa walioanza kupata msukosuko wa kisiasa kwa maelekezo ya Pareso, ni pamoja na Katibu wa Madiwani wa mkoa wa Arusha na diwani wa Viti Maalum, wilayani Karatu, Sabina Marmo.

Sabina ambaye Jumamosi iliyopita, alijitosa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karatu, sasa anasukiwa zengwe la kufukuzwa kwenye chama hicho.

Katika uchaguzi huo, Sabina aliyeonekana kuungwa mkono na kundi kubwa la madiwani, alipingwa kwa nguvu zote na Pareso na Jubleti.

Inaelezwa kuwa Jubleti alihakikisha Sabina hachaguliwi kwenye nafasi hiyo kwa kushawishi baadhi ya madiwani kwa ahadi kuwa wakifanya hivyo, atawapanga kwenye kamati ya fedha.

Naye Pareso aliagiza madiwani watatu wa Viti Maalum, Sophia Shauri, Cristine Safari na Levina Emmanuel, kutomchagua Sabina kwa madai kuwa nitishio kwa harakati zake za “kumng’oa Qambalo 2020.”

Mwandishi wa gazeti hili ameshindwa kumpata Pareso, kuzungumzia suala hilo. Alipotafutwa kwenye simu yake ya mkononi, mara zote simu hiyo ilikuwa inaita bila kupokelewa.

Lakini mmoja wa madiwani hao watatu ambaye amezugumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, ameeleza kuwa ni kweli kwamba Pareso alitoa maelelezo kwao wasimpigie kura Sabina.

Diwani huyo alisema yeye anamuunga mkono Sabina kwa kuwa ni mwanamke mwenzake, aliyejitokeza mwanzo kumwomba kura ambaye anaamini alikuwa ma uwezo wa kushika nafasi.

Alisema alishindwa kumpigia kura Sabina kwa kuwa mbunge huyo alisisitiza sana kwamba kumchagua Sabina ni kumsaliti yeye.

Sabina alishndwa katika uchaguzi huo na Simon Lazaro Bajuta aliyepata kura 7 huku yeye akipata kura 5.

Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa vipindi vitatu mfululizo, Lazaro Massay, amethibitishia MwanaHALISI Online kuwa kuna hatari ya Chadema kupoteza halmashauri ya Karatu.

“Hapa Karatu kuna mgogoro mkubwa wa uongozi ndani ya Chadema. Nimewahi kumueleza haya mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe. Nimeeleza haya wakati nikiwa mjumbe wa Kamati Kuu, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa,” anaeleza.

Anasema, “mimi siogopi kusema ukweli. Nawambia kabla ya mambo hayajaharibika, wachukue hatua. Vinginevyo, huyu Jubleti na mheshimiwa Pareso, watakizika Chadema hapa Karatu.

“Mtu mwenye akili timamu, hawezi kumpinga mbunge ambaye hajamaliza kipindi chake na ambaye anakubalika kwa wapigakura wake wake. Pareso anayafanya haya hadharani. Anapinga hata wanawake wenzake kuwa viongozi, wakati yeye ni mwenyekiti wa Bawacha wa wilaya hiyo.”

Lazaro ambaye kwa sasa anasema alikuwa amejipumzisha na siasa za Karatu anadai kuwa ameamua kusema hayo kwa kuwa anauchungu na Chadema. Anasema ameijenga Chadema kwa muda mrefu, lakini anaona sasa inapasuliwa kutokana na maslahi binafsi.

“Mimi ni mmoja wa wasisi wa chama hiki. Sitakubali kukiona kinasambaratika. Nimeongoza halmashauri ya Karatu kwa miaka 15, tena kwa mafanikio makubwa. Siko tayari, nitasema hadi dakika za mwisho,” ameeleza

Jimbo la Karatu limekuwa ya chadema kwa miaka 25 sasa; tangu wakati wa Dk. Wilbroad Slaa aliyekuwa Mbunge wa Karatu kwa vipingi vitatu mfululizo, Katibu Mkuu wa Chadema kwa miaka 20 na ambaye amepata kugombea Urais wa Jamhuri Muungano.

Ikiwa Chadema itapoteza halmashauri ya Karatu basi litakuwa pigo kubwa kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!