Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema ilivyopoteza wabunge 17
Habari za SiasaTangulizi

Chadema ilivyopoteza wabunge 17

Spread the love

MBUNGE wa Kilombero, Kusini Mashariki mwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Peter Ambrose Lijualikali (35),  amekuwa mbunge wa 17 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuondoka bungeni, kujiengua ama kupoteza sifa za kuwa mbunge. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Lijualikali alitangaza kuondoka Chadema, jana Jumatatu, tarehe 18 Mei 2020. Haijafahamika hadi sasa, kwamba mpaka mkutano huu wa 19 wa Bunge unamalizika, Chadema kitabaki na wabunge wangapi.

Katika uchaguzi mkuu uliyopita, Chadema kilifanikiwa kujikusanyia wabunge 71, ambako kati yao, wabunge wa majimbo walikuwa 35 na wa Viti Maalum 36.

Hata hivyo, hadi leo Jumanne, tarehe 19 Mei 2020, chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimejikuta kikipoteza wabunge wake 17 wa majimbo kwa sababu tofauti. Kwa sasa, Chadema kimebakiwa na wabunge 18 pekee wa majimbo.

Kati ya wabunge hao 17 waliopoteza ubunge, wapo waliojiuzulu wenyewe kwa kutangaza kukihama chama hicho; wapo waliofukuzwa kwenye chama; wapo waliovuliwa ubunge na mahakama, yupo aliyefariki dunia, wapo waliong’olewa bungeni na Spika na yupo aliyevuliwa ubunge na mahakama.

Katika orodha hiyo ya wabunge 17 kati yao saba walijiuzulu kwa nyakati tofauti katika kile walichokiita, “kuunga mkono” juhudi zinazofanywa na serikali ya Rais John Magufuli.

Baada ya kuondoka Chadema na kujiunga na CCM, walipitishwa na kugombea tena katika majimbo hayohayo na kuibuka washindi, huku wengine wakipita bila kupingwa.

 

Miongoni mwa wabunge waliondoka wenyewe ndani ya Chadema, ni pamoja na Julius Kalanga (Monduli); Ryoba Marwa (Serengeti); Joseph Mkundi (Ukerewe); James Ole Millya (Simanjiro) na Pauline Gekul (Babati Mjini).

Wengine, ni Mwita Waitara (Ukonga), Dk Godwin Mollel (Siha).

Anthony Komu, aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Moshi Vijijini na Joseph Selasini, aliyekuwa mbunge wa Rombo, walitangaza kuondoka Chadema na kujiunga na NCCR- Mageuzi. Wakasema, watabaki Chadema hadi kumalizika kwa muda wa ubunge wao na kwamba watagombea tena nafasi hiyo, kupitia chama chao hicho kipya.

Tundu Lissu, aliyekuwa mbunge wa chama hicho katika jimbo la Singida Mashariki na Joshua Nassari, aliyekuwa mbunge wa Arumeru Mashariki, walipoteza nyadhifa zao kwa kuvuliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Katika maelezo yake, Spika Ndugai alisema, Lissu na Nassari wamepoteza sifa za kuwa mbunge kwa kuwa wamekuwa “watoro bungeni.”

Uchaguzi ulipotangazwa wa Arumeru Mashariki, Chadema na baadhi ya vyama vya upinzani havikushiriki vikidai mazingira ya uchaguzi si sawa; hivyo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pallangyo.

Kauli hiyo ya Spika Ndugai kuhusu Lissu, ilipingwa na Lissu mwenyewe na chama chake, kwa maelezo kuwa mwanasiasa huyo, aliondoka nchini kueleka Nairobi, nchini Kenya, akiwa mahututi, kufuatia kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana.”

Shambulio dhidi ya Lissu lilitokea nyumbani kwake, maeneo ya Area D, mjini Dodoma, tarehe 7 Septemba 2017.

Siku hiyo hiyo usiku, Lissu alisafirishwa kwenda Nairobi, kwa matibabu zaidi. Alianzia safari yake, kutokea hospitali ya Rufaa mjini Dodoma.

Alipata matibabu Nairobi hadi tarehe 6 Januari 2018 alipohamishiwa nchini Ubelgiji. Mpaka sasa, Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), bado yuko nchini humo, akinusuru maisha yake.

Kama ilivyokuwa Arumeru, uchaguzi ulipoitishwa kwenye jimbo la Singida Mashariki, chama chake, hakikushiriki uchaguzi huo, jambo ambalo lilimfanya mgombea wa CCM, Miraji Mtaturu, kupita bila kupingwa.

Mbunge aliyefariki dunia, ni Kasuku Bilago, aliyekuwa mbunge wa Buyungu mkoani Kigoma. Bilago alikutwa na mauti, mchana wa tarehe 26 Mei 2018, akiwa katika hospitali ya taifa Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Uchaguzi wa marudio ulipofanyika, aliyeibuka mshindi alikuwa Christopher Chiza (CCM).

Naye Onesmo Ole Nangole, aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Longido mkoani Arusha, alivuliwa ubunge wake na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Katika maamuzi yake, mahakama hiyo ilisema, kulikuwa na matumizi yasiostahili kutumika kujazwa matokeo ya ubunge, kwa kutumia fomu namba 21c za kujaza matokeo ya udiwani na kujaza matokeo ya Ubunge, badala ya kutumia fomu namba 21b.

Uchaguzi ulipotangazwa tena, Chadema haikushiriki, jambo ambalo lilisababisha mgombea wa CCM, Dk. Steven Kiruswa kuibuka mshindi. Katika uchaguzi wa awali wa 25 Oktoba 2015, Dk. Kiruswa alishindwa na Nang’ole, jambo lililomfanya kukimbilia mahakamani.

Aidha, Cecil Mwambe aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Ndanda, yeye alitangaza kuondoka chama hicho, tarehe 15 Februari 2020 na kujiunga na CCM.

Hata hivyo, Mwambe ameshindwa kurejea bungeni, kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, uchaguzi mdogo hauwezi kufanyika ikiwa kumesalia chini ya miezi 12 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Katika maelezo yake, Lijualikali alisema, ameondoka Chadema kukimbia unyanyasaji aliyodai umekithiri ndani ya Chadema. Ameomba kupewa fursa ya kupokelewa ndani ya CCM.

Kuondoka kwa Lijualikali kunatokana na maamuzi ya Kamati Kuu ya Chadema, iliyokutana tarehe 9 na 10 Mei 2020, kufikia maamuzi ya kutaka yeye na wenzake 14 wajieleze.

Chadema ilichukua uamuzi huo kufuatia uamuzi wa wabunge hao, kuhudhuria mkutano wa Bunge, kinyume na kile kilichodaiwa, kutotekeleza “maelekezo ya viongozi.”

Ni mkutano huo huo wa Kamati Kuu, ndio umefikia maamuzi ya kuwafukuza, Komu,Selasini, David Silinde, mbunge wa Momba na Willfred Lwakatare, mbunge wa Bukoba Mjini.

Lwakatare tayari alishatangaza kutokugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!