Monday , 11 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema: Hatujapokea hata senti moja ya ruzuku
Habari za Siasa

Chadema: Hatujapokea hata senti moja ya ruzuku

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Rodrick Lutembeka
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kimekana taarifa kuwa kimekuwa kikipokea ruzuku ya mamilioni ya shilingi kutoka serikalini, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa chama hicho, Rodrick Lutembeka, ameliambia MwanaHALISI Online, leo Ijumaa, tarehe 29 Januari 2021, kuwa chama chake hakijapokea hata shilingi kutoka serikalini kama mgawo wake wa ruzuku.

Amesema, “…hakuna hata senti moja iliyoingia Chadema ya ruzuku. Nawaomba muulizeni huyo anayesema, tumepokea fedha ya ruzuku, kwamba alitupa lini.”

Mbali na kutaka anayetoa taarifa kuwa Chadema kimepokea fedha hizo, Lutembeka ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Chadema, ametaka mhusika kuuhakikisha umma ukweli wa madai hayo kwa kuanika ushahidi wa jambo hadharani.

Lutembeka amesema, msajili wa vyama vya siasa anapaswa kueleza kama ametoa hizo fedha, aeleze ni kiasi gani lakini “tunachojua sisi, hakuna fedha iliyoingia.”

Gazeti moja la kila wiki lenye mwelekeo wa “kukishughulikia Chadema,” limeandika leo Ijumaa, kuwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimekuwa kikipokea ruzuku kutoka serikalini, na kwamba sehemu ya fedha hizo, ndizo zinazotumika kugharamia kikao cha Kamati Kuu (CC), kinachofanyika Zanzibar.

Chadema kimetangaza kususia ruzuku na vyote vinavyopatikana kupitia uchaguzi mkuu uliyopita, ikiwamo ubunge wa viti maalum na kueleza kuwa hakitambui matokeo ya uchaguzi huo na mchakato wake.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, kufuatia msimamo huo, Chadema kimegoma kupeleka kwa msajili wa vyama, jina la akaunti ya Baraza la Wadhamini, ili kuweza kuingiziwa fedha zake.

Kwa mujibu wa taratibu za utoaji wa ruzzuku kwa vyama vya siasa, kila baada ya kumalizika uchaguzi mkuu, ofisi ya msajili hukokotoa hesabu ya kura za jumla za kila chama cha siasa kilichoshiriki uchaguzi, ili kupata hesabu kamili ya fedha ambayo vyama ambavyo vimekidhi vigezo, vinapaswa kupata.

Aidha, baada ya mchakato huo, kila chama cha siasa, hujulishwa kiasi ambacho kinapaswa kupokea na kisha kutakiwa kuwasilisha kwa msajili, jina la akaunti itakayotumika kupokelea fedha.

Fedha ambayo hutumika kupokea ruzuku, ni ile iliyofunguliwa na Baraza la Wadhamini, ambapo baada ya kupokea fedha hizo, huzipeleka kwenye akaunti ya chama kwa ajili ya kuzitumia kwa maelekezo ya maamuzi ya vikao vyake.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema, “Chadema ni chama cha siasa na hivyo, ni taasi ya umma. Kama kuna hela imeingia kwenye chama, ni muhimu msajili wa vyama akatoa ushahidi ili kulinda fedha za wananchi.”

Amesema, kitendo cha baadhi ya magazeti kung’ang’ania kuwa Chadema kimepokea ruzuku wakati viongozi wenyewe wamekuwa wakikana, kinalenga kuleta chokochoko kwenye chama, jambo ambalo halina afya kwa chama na taifa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Biteko: Samia ni muumini wa maridhiano sio kwa kuigiza

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mpango: Sitakufa bali nitaishi

Spread the loveMAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mbowe: Miaka 62 ya uhuru tujenge upya mioyo yetu

Spread the loveWAKATI Tanganyika ikiadhimisha miaka 62 tangu kupata uhuru, Mwenyekiti wa...

Habari za Siasa

Rais Samia asamehe wafungwa 2,244

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewasamehe wafungwa 2,244, huku akiwabadilishia...

error: Content is protected !!