March 3, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema Dodoma wamtetea Lissu

Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Singida, akiwasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu

Spread the love

CHAMA Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kanda ya kati kimelaani kitendo cha jeshi la polisi nchini kumkamata mara kwa mara, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), anaandika Dany Tibason.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Alphonce Mbassa amesema kitendo cha polisi kumkamata mra kwa mara ni sawa na serikali kushindwa kufanya siasa za vyama vingi.

Amesema kwa kuwa kuna dalili hizo za kushindwa ni bora ipeleke muswada bungeni ili kuvifuta kabisa visiwepo.

“Kamwe siasa za chuki haziwezi kujenga nchi bali nchi inajengwa kwa siasa zenye hoja na tabia ya kuwakamata wapinzani mara kwa mara na kuwaweka ndani huku wanasiasa wa chama watawala wakiendelea kufanya ndivyo sivyo ni chuki za wazi,” amesema

Naye mwenyekiti wa baraza la vijana mastaafu mkoa wa Dodoma(Bavicha), Malambaya Manayanya amesema kwa sasa inaonekana wazi kuwa serikali inatumia jeshi la polisi kukandamiza upinzani.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Dodoma pamoja na wanasiasa kutoka vyama vya siasa wamesema kwamba wanakerwa na vitendo vya jeshi la polisi kumkamata mara kwa mara Lissu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema kitendo cha kukamatwa mara kwa mara kinaonyesha kwamba mwanasiasa huyo ni tishio.

Wamesema kuendelea kumkamata ni sawa na kumpa umaarufu na kwamba jamii itaendelea kaumini maneno anayosema yana ukweli.

error: Content is protected !!