August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema, CCM wazichapa; visu, mawe vyatumika

Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, akipokea kadi na bendera ya Chadema katika kampeni za 2015

Spread the love

CHUKI na visasi kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeendelea kumea baada ya wafuasi wa vyama hivyo kuchapana makonde mkoani Morogoro, anaandika Christina Haule.

Wanachama hao wamechapana makonde kwenye kampeni za udiwani zinazoendelea mkoani humo huku watu wanne wakijeruhiwa.

Vurugu hizo zilitokea katika eneo la Lukwangule karibu na Ofisi za CCM ambapo maandamano ya wafuasi wa vyama hivyo viwili yalikutana.

Baada ya wafuasi hao kukutana eneo hilo jana saa moja jioni, walianza kurushiana vijembe na maneno ya kejeli jambo ambalo liliwapandisha jazba na kuanza vurugu ambapo silaha zilizotumika ni mapanga, bakora na mawe.

CCM wakiwa na gari lao la matangazo wakiendelea kupiga nyimbo za hamasa na kusifu chama hicho, walikutana na gari la Chadema wakiwa na wafuasi wao ambao nao walikuwa wakipiga nyimbo za kuhamasisha wanachama wao na hapo ndipo walioanza kurushiana vijembe.

Maulidi Chambilila ambaye ni Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi CCM Mkoa wa Morogoro amesema, vurugu hizo pia zilisababisha majeraha kwa watu wanne miongoni mwao akiwa Lukoo Chingwi aliyepasuliwa sehemu ya kichwa chake kwa jiwe.

Kwenye vurugu hizo pia Tausi Said alijeruhiwa kwenye mbavu kwa kupigwa kwa fimbo pamoja na jiwe huku Gerald Jeilaikai akichomwa kisu cha mbavu na Kurwa Hanu aliyejeruhiwa kwa jiwe kisogoni.

Shaaban Dimoso, Katibu Mwenezi wa Chadema Mkoa wa Morogoro alitoa shutuma kwa CCM akisema, ndio walioanzisha vurugu kwa kutegemea kulindwa na dola.

Amesema kuwa, CCM walianza vurugu kwa kuwarushia mawe wafuasi wa Chadema jambo lililosababisha nao kujibu mashambulizi hayo.

Katika mikoa mbalimbali nchini tarehe 22 Januari mwaka huu kunatarajiwa kuwa na uchaguzi mdogo wa udiwani ambapo visiwani Zanzibar kutakuwepo na uchaguzi ubunge katika Jimbo la Dimani.

error: Content is protected !!