January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chadema: CCM iache kuweweseka

Kikosi cha ulinzi cha Chadema

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kauli ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kulalamikia mafunzo ya maadili ya uzalendo kwa vijana wao maarufu kama “Red Brigade”, ni hatua ya kuweweseka. Anaandika Mwandishi wetu(endelea).

Msimamo wa Chadema unatolewa siku moja tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, akaririwe na vyombo vya habari wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, akidai kuwa Red Brigade imefunzwa “ugaidi” wa kuteka, kutesa watu na kuvuruga amani.

Kwa mujibu wa Tumaini Makene- Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, CCM kwa mara nyingine tena kimerudia kutoa kauli kuhusu mafunzo hayo ya uzalendo kwa nchi, ukakamavu na kuwandaa vijana wa chama katika misingi ya uongozi.

“Tunatumia fursa hii; kwanza kufafanua dhana ya mafunzo hayo wanayopewa vijana wa Chadema, pili kuwasaidia CCM kujua adui yao halisi atakayewaondoa madarakani mwaka huu.

“Tatu kuendelea kuwatia shime Watanzania kusimamia masuala ya msingi yanayolikabili taifa kwa kuelewa malengo ya propaganda za Abdulrahman Kinana na Nape Nnauye wanazofanya kupitia mikutano ya hadhara,” amesema Makene.

Amesema kama inavyojulikana, msingi wa mafunzo kwa vijana wa Chadema yanayoendelea nchi nzima kupitia njia ya makongamano ya wazi uko katika Katiba ya chama ibara ya 7.7.5 inayosema;

“Kutakuwa na mfumo wa ulinzi na usalama wa mali, viongozi na maslahi ya chama utakaotambulika kama Brigedia Nyekundu (Red Brigade).”

Makene ameongeza kuwa lengo kuu la mafunzo haya ni kuwapatia vijana hao maarifa juu ya maadili ya uzalendo kwa nchi kama vile kulinda rasilimali za nchi, kupiga vita ufisadi na rushwa na kuwaandaa katika misingi ya uongozi ndani ya jamii.

“Makongamano ya mafunzo hayo yanafanyika kwa uwazi. Vyombo vya habari vinakaribishwa kwa ajili ya kuuhabarisha umma. Maofisa wa Serikali wanakaribishwa kutoa mada.

“Mathalani wakati wa kongamano la namna hiyo Jimbo la Solwa, uongozi wa chama katika eneo hilo ulipeleka mwaliko Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ili atoe mada ya ulinzi shirikishi kwa vijana wale,”amesema.

Makene amefafanua kuwa mambo yote yamekuwa yakizungumzwa mbele ya hadhara, vyombo vya habari vimeripoti, lakini jambo la kushangaza ni CCM kupata kiwewe na kuyaita mafunzo hayo kuwa ya “kigaidi”.

“Jibu lake liko wazi, CCM chama kilichogeuka kuwa mwamvuli wa mafisadi na mbolea inayomea ufisadi, hakiwezi kufurahia kuona vijana wakipewa mafunzo ya uzalendo kwa nchi yao,” amesema na kuongeza;

Chama kilichohakikisha kinaondoa uadilifu, uwazi na uzalendo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba mpya, hakiwezi kukubali vijana ambao ni moja ya nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa na ujenzi wa demokrasia imara, wapewe mafunzo yatakayowasaidia kusimamia haki na kupinga dhuluma katika nchi.

Kwa mujibu wa Makene, propaganda za Nape ni moja ya mikakati iliyojadiliwa na kupitishwa na Kamati Kuu ya CCM hivi karibuni kwa lengo la kupumbaza watu wasiiunge mkono Chadema.

“Kama kweli ‘vikosi’ vya ulinzi ni tishio kwa nchi, CCM ndiyo ilipaswa kuwa ya kwanza kuacha kuwapatia vijana wake wa Green Guard mafunzo ya kijeshi kwenye makambi ya siri, yanayohusisha matumizi ya silaha,” amesema Makene.

error: Content is protected !!