Tuesday , 5 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mwambe: Nataka kumtua mzigo Mbowe, Ajifananisha na Simon Wakirene aliyemtua Msalaba Yesu
Habari za SiasaTangulizi

Mwambe: Nataka kumtua mzigo Mbowe, Ajifananisha na Simon Wakirene aliyemtua Msalaba Yesu

Cecil Mwambe,, Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Ndanda, mkoani Mtwara,
Spread the love

MBUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Ndanda, mkoani Mtwara, Cecil Mwambe, amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti ndani ya chama chake. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Anasema, ameamua kugombea nafasi hiyo ili kumpungumzia mzigo mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Anasema, “nimeamua kujitolea kufanya kazi ya Simon Wakirene, ndani ya chama changu ya kumpokea mwenyekiti wangu wa sasa, Freeman Mbowe, kazi ya uongozi ndani ya chama.”

Anasema, “siku zote, mwenyekiti wetu amekuwa akisema, ‘kazi hii ya kuongoza chama ni ngumu mno.’ Amekuwa akieleza, kwamba akipatikana mtu mwingine, yuko tayari kumtulia mzigo huu. Sasa mimi nimejitokeza kumpokea zigo hili, mithili ya Simon Wakirene, alivyompokea Bwana Yesu Msalaba.”

Mwambe alitoa kauli hiyo leo, tarehe 26 Novemba 2019, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, katika hoteli ya Grandview, iliyopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Taarifa kuwa Mwambe amejitosa katika kinyang’anyiro hicho, zimekuja siku moja, baada ya Mchungaji Peter Msigwa, kusambaza andiko refu linalotuhumu wabunge wawili wa Chadema, Anthony Komu (Moshi Vijijini) na Saed Kubenea (Ubungo), kuwa ni miongoni mwa wanaopanga mkakati wa kumuondoa Mbowe kwenye kiti cha uenyekiti.

Uchaguzi mkuu wa chama hicho cha upinzani nchini, umepangwa kufanyika tarehe 18 Desemba mwaka huu.

Akizungumza kwa kujiamini na kujibu hoja moja baada ya nyingine, Mwambe amesema, “…nimeona haja ya kugombea baada ya kumshuhudia mwenyekiti wetu wa chama Mbowe, akitishia kuachia nafasi hiyo kwa zaidi ya mara tatu.”

Amesema, “nimeona iko haja ya kumpokea kijiti hasa baada ya kueleza kwa kina madhira aliyopitia kwa vipindi vilivyotangulia. Nimeingiwa na huruma. Ninafahamu kuwa Mbowe amefanya mengi mazuri kwa chama chetu; ila kama binadamu huchoka na kuhitaji usaidizi.”

Mbunge huyo pekee wa Chadema katika mikoa ya Kusini amesema, kingine kilichomsukuma kuchukua hatua hiyo, ni kuenzi na kuishi dhana ya demokrasia inayobeba jina la Chadema, pamoja na kuweka ushindani katika kupata viongozi bora.

“Uchaguzi usio na ushindani hutoa viongozi ambao mwisho wa siku hudai kuwa walishurutishwa kugombea. Ushindani hukuza ubunifu na ushindani hukuza demokrasia,” ameeleza.

Kuhusu madai kuwa amekuja Chadema kuja kuwavuruga na  kumpindua Mbowe, mwanasiasa huyo, haraka alisema, “kama madai hayo yangekuwa na cheme ya ukweli, uongozi wa chama hiki, ungekwisha kunichukulia hatua, kwa kuwa ni ukiukaji wa katiba.”

“Hakuna mpango wa kuvuruga chama. Hayo ni maneno ya washindani wangu waliojawa na hofu na woga wa uchaguzi,” ameeleza Mwambe na kuongeza, “tunapokuwa katika vyama, hakuna nafasi ya kuchaguliana rafiki.”

Mwambe amesema tuhuma zinazoelekezwa kwake, ikiwemo kukaidi kutotoa sehemu ya mshahara wake wa Bunge kuchangia chama, si za kweli, na kwamba zinatokana na kampeni chafu za uchaguzi huo.

Ameeleza kuwa, nyaraka inayoonesha kwamba hajachangia, imetoka kipindi hiki ambacho ametangaza kugombea uenyekiti, ili kumchafua.

Amesema, “nyaraka inayoonesha sikuweza kuchangia michango kikatiba, ni kutokana na figisu zilizotokea ndani ya chama changu. Ilitolewa siku 10 kabla sijatangaza kugombea. Wasiotaka nigombee ndio waliofanya hivyo ili kunichafua. Nadhani hawakufanikiwa.”

Mwambe amekuwa mwanasiasa wa kwanza ndani ya Chadema, kujitokeza hadharani kutangaza na hatimaye kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti wa Mbowe. Haijulikani nani wengine wanaweza kufuta nyayo zake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Biteko: Viongozi tuache alama nzuri katika utendaji wetu

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Chanzo maporomoko yaliyoua 65 Hanang, chatajwa

Spread the loveSERIKALI imesema kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang ambao ilikuwa...

Habari za Siasa

Baba yake Ole Sabaya ashinda Uenyekiti CCM – Arusha

Spread the loveLoy Thomas Sabaya ambaye ni Baba wa aliyekuwa Mkuu wa...

Habari za Siasa

Serikali yaagiza uchunguzi chanzo maporomoko Hanang

Spread the loveSERIKALI imeagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha maporomoko ya...

error: Content is protected !!