January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CDA yazidi kumtafuna mbunge wa CCM

Spread the love

MZIMU wa mgombea Ubunge jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (CCM) kuwa ni wakili wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), umezidi kumwandana licha ya kujitetetea mara kwa mara kuwa hahusiki. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mavunde, ambaye ni mwanasheria kitaaluma anadaiwa kushirikiana na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), kuwabomolea wananchi nyumba zao bila ya kufuata utaratibu wa kuyafanyia tathimini kisha kwalipa fidia.

Kauli hizo zimekuwa zikitolewa katika mikutano ya mbalimbali ya kampeni ya kuwania ubunge katika jimbo la Dodoma Mjini huku mgombea Ubunge wa Chadema, Benson Kigaila na aliyekuwa kampeni meneja wa Mavunde wakati wa kura za maoni Sospeter Mzungu wakiweka jambo hilo hadharani.

Mzungu, ambaye anatumia majukwaa ya kampeni za Chadema, amesema kuwa Mavunde ni miongoni mwa wanasheria ambao wanalipwa fedha nyingi na CDA kwa ajili ya kuwafanya wananchi waporwe maeneo yao bila kulipwa fidia.

“Mimi nilikuwa kampeni meneja wa Mavunde wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, pamoja na mambo mengine nilibahatika kuona mikataba mbalimbali ambayo CDA na Mavunde walikubaliana ili awasaidie kisheria pale wanapokuwa wakibomoa nyumba za wananchi wa maeneo mbalimbali katika Manispaa ya Dodoma.

“Mikataba hiyo ninayo na kama Mavunde anakata kuwa hausiki moja kwa moja na watu wa CDA anipeleke mahakamani, Mavunde ni moja ya kikwazo katika maendeleo ya mji wa Dodoma hivyo iwapo atakuwa mbunge wananchi wote wenye matatizo ya ardhi wataendelea kuwa watumwa katika maeneo yao au kufukuzwa kabisa,” alieza Mzungu.

Katika mikutano yake Kigaila amesema jimbo la Dodoma linahitaji mbunge ambaye ni mtetezi wa wanyonge ambapo alibainisha kuwa yeye anafaa baadala ya mtu ambaye anaweza kuja kuwakandamiza wananchi.

Akizungumzia masula ya ardhi, Kigaila amesema wakazi wa Manispaa ya Dodoma wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutomiliki ardhi kutokana na urasimu wa CDA.

“Nyie wananchi wa Dodoma mnajua jinsi nilivyo wapigania wakati mkivunjiwa nyumba zenu na bila kupewa dhamana kumbuka nimewekwa ndani mara kadhaa lakini mnasikia mwenzagu mgombea wa CCM anavyobebana na watu wa CDA, Je mnadhani mtapona mkimchagua.

“Kama ameonesha kushirikiana na CDA ambayo inawatesa na kuwanyanyasa, Je akiwa mbunge na anaingia moja kwa moja kuwa mjumbe wa bodi mnategemea nini hapo, nipeni kura wana wa Dodoma tubadilishe jimbo hili ambayo imekuwa ikiitwa makao mkuu bila mafanikio,” amesema Kigaila.

Pamoja na kauli hizo zinazotolewa dhidi yake, Mavunde amesema hajawahi kuwa mwanasheria wa CDA licha ya kuwa yeye ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea.

“Mimi sijawahi kushiriki kazi na CDA hayo ni maneno ya kisiasa tu mimi ni wakili wa kujitegemea na nafanya kazi zangu nje ya CDA na ikumbukwe pia nilikuwa mkuu wa Wilaya ya Mpwpwa,” alijieleza Mavunde.

Ofisa habari wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA), Angela Msimbila alipoulizwa kama kweli Mavunde alishawahi kuwa wakili wa mamlaka hiyo, amesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwani yanawahusu wanasiasa, yabaki kuwa ya wanasiasa.

“Sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu hatufanyi mambo kisiasa wala atutekelezi matakwa ya wanasiasa hivyo sitaki kuzungumza jambo lolote juu ya mambo hayo,” amesema Msimbila.

error: Content is protected !!