August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CDA bado ‘pasua kichwa’ Dodoma

Antony Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini

Spread the love

MAMLAKA ya Ustawi wa Makao ya nchi – Dodoma (CDA), imeendelea kutupiwa lawama kwa madai ya kuwapora ardhi wananchi na kuiuza kwa wageni wanaohamia katika mji huo, anaandika Dany Tibason.

Wanaolalamika kuibiwa maeneo yao na CDA ni wakazi wa Kata ya Tambuka reli katika Manispaaa ya Dodoma, wametoa madai hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya mikutano vilivyopo katika kata hiyo.

Wananchi hao wametoa malalamiko hayo mbele ya Antony Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri katika Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu aliyekuwa ameitisha mkutano wa hadhara ili kujadili suala hilo.

Andason Ndoji aliyejitambulisha kama mmoja wa wahanga wa utendaji wa CDA amesema mamlaka hiyo imekuwa ikichukua maeneo yao na kuyauza kwa bei kubwa tofauti na fidia wanayowapa wananchi ambao wanamiliki mashamba hayo.

“CDA inatupora wananchi mashamba yetu halafu inayauza kwa watu wengine kwa bei kubwa na sisi ambao ni wamiliki halali wa mashamba hayo tunanyimwa fidia na tukidai sana tunapewa fidia kidogo sana,” amesema.

Naye Makrina Lombida mkazi wa manispaa hiyo amesema ameporwa kiwanja na CDA jambo lililomsababishia umasikini mkubwa kutokana na kushindwa kufanya shughuli zake za kila siku ambazo zilikuwa zikimpatia kipato kupitia shamba hilo.

Kwa Upande wake Msahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jafari Mwanyemba akijibu hoja za wananchi hao amesema ni kweli changamoto ya viwanja ni kweli kutokana na kuwa anayemiliki viwanja kwa sasa ni CDA.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma alipoulizwa kuhusu madai hayo ya wananchi amesema kazi ya kupanga mji ni ya CDA lakini akadai kuwa kutokana na malalamiko ya kuuzwa kwa viwanja vya wananchi CDA itawafidia wananchi kwa kuwapa maeneo mengine watakayokuwa wameyachagua.

CDA imekuwa ikitupiwa lawama na wananchi wengi wa mji wa Dodoma kwa muda mrefu, ikidaiwa kuuza maeneo ya wananchi bila ridhaa yao na kulipa fidia ndogo isiyoendana na ukubwa wa eneo lililouzwa. Mamlaka hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuupangilia mji wa Dodoma ili uweze kuwa makao makuu ya nchi.

error: Content is protected !!