January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yazidi kutengwa Z’bar

Spread the love

ORODHA ya vyama vinavyopingana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kurudia uchaguzi visiwani Zanzibar inazidi kuongezeka, anaandika Happyness Lidwino.

Chama cha ACT-Wazalendo kimeingia kwenye orodha ya vyama vinavyopinga marudio hayo na kufanya idadi ya vyama vinavyogomea kuongezeka na kuwa tisa kati ya 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi huo wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

ZEC ilitangaza marudio ya uchaguzi huo kuwa tarehe 20 Machi mwaka huu baada ya mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana kwa madai ya kugubikwa na kasoro.

Hatua hiyo imepingwa na baadhi ya wananchi, wanataaluma, wanasisa na taasisi ndani ya nchi pia mataifa ya nje ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) pia Marekani.

Kwenye uchaguzi huo wa awali, Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alitangaza matokeo yake yaliyoonesha kuwa amemshinda mpinzani wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi visiwani humo.

Kauli ya ACT-Wazalendo imetolewa na Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama hicho baada ya kuwepo kwa makubaliano yaliyofanyika kwenye Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilihitimishwa jana Jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo imetoa msimamo wa kutoshiriki uchaguzi huo na kutoa wito kwa Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania kuchukua hatau stahiki kwa mamlaka aliyopewa kikatiba kuliko kukimbia jukumu lake.

Akizungumza na waandika ofisini kwake Zitto amesema, Kamati Kuu pia inataka madiwani na wawakilishi walioshinda katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana kutangazwa na ZEC ili watambulike na kuanza kuwatumikia wananchi.

Zitto amesema, Kamati Kuu imeendelea kusisitiza kuwa Jecha hakuwa na uhalali wa kisiasa, kikatiba na kisheria kuufuta uchaguzi Zanzibar.

“Dalili zote za kisiasa zinaonesha kuwa Jecha alichukua hatua ile kwa shinikizo au kwa mapenzi ya kisiasa kwa lengo la kuzuia ushindi wa chama kimoja ambacho kilikua na dalili ya kushinda.

“Mbali na CCM, waangalizi wote wa uchaguzi wa ndani na nje pamoja na jumuiya za kimataifa wametamka bayana kwa uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika kwa haki, huru na demokrasia na matokeo ya uchaguzi huo yalizingatia utashi wa wapiga kura,” amesema Zitto.

“Kamati kuu pia tunaamini kwamba suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar ni kufanya mazungumzo yatakayojumuisha wadau wote muhimu katika mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar. Hatuamini kwamba mkwamo huu utatatuliwa kwa vitisho vya dola,” amesema.

error: Content is protected !!