November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

CCM yazibana wizara 3 misitu ya hifadhi

Moja ya misitu iliyopo nchini Tanzania

Spread the love

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kukutana na kufanya mapitio kuhusu misitu ya hifadhi iliyopo wilayani Tanganyika mkoani Katavi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Katavi … (endelea).

Agizo hilo limetolewa juzi wilayani Tanganyika mkoani Katavi na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alipozungumza na wazee wa wilaya hiyo katika ziara ya Sekretarieti ya NEC iliyofika mkoani humo kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na uimara wa chama mashinani.

Alisema uwepo wa misitu katika wilaya hiyo, uwe ni neema na kuleta manufaa kwa wananchi.

“Maelekezo ya chama ni kwamba wizara hizi zikutane, zijadili kwa pamoja suala hili na kuja na mwafaka wa pamoja kuhusu misitu iliyopo Tanganyika,” alisema na kuongeza

“Lengo letu ni kuona tunaitunza kwa ajili ya ustawi wa mazingira yetu, kuchochea utalii lakini kubwa zaidi, ni lazima wananchi wanufaike nayo,” alisema.

Shaka alitoa maelekezo hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa kulinda na kuihifadhi misitu ya Nkamba, Tongwe Mashariki na Tongwe Magharibi.

Katibu wa Itikadi na uenezi CCM, Shaka Hamidu Shaka

Hatua hizo zinadaiwa kuwabana wananchi katika baadhi ya maeneo kuwa na eneo dogo la kufanyia shughuli zao za kiuchumi kikiwemo kilimo.

Shaka aliitaka wadau hao kukutana na kujadili vifugu mbalimbali vya kisheria vinavyohusika katika uhifadhi misitu na kutwaa maeneo kwa ajili ya uhifadhi na kuhakikisha sheria zinazingatiwa.

Awali akitoa maelezo juu ya msitu huo katika Kijiji cha Kasekese, katika Jimbo la Mpanda Vijijini wilayani Tanganyika, Mbunge wa Jimbo hilo, Moshi Kakoso, alisema Juni 25, mwaka huu serikali kupitia tangazo namba 460 imeanzisha eneo jipya la pori la akiba linaloitwa Luganzo-Tongwe katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakimilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Alisema tangazo hilo jipya limechukua eneo lote la Msitu wa Tongwe Mashariki wenye hekta 167,832 sawa na ekari 414,720.

Kakoso alisema tangazo hilo pia limeingilia eneo la Luhafwe lililotengwa na Halmashauri ya Wilaya hiyo, kwa ajili ya uwekezaji wa kiuchumi.

Kakoso alisema kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza, ni vyema ukawekwa utaratibu wa kuhakikisha wananchi wananufaika.

Akiwa katika eneo la ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Karema wilayani humo, Shaka aliipongeza serikali kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kifungu cha 59 ibara ndogo (b) na (v) inayosisitiza kuhusu ujenzi wa miundombinu hususani ya bandari.

Alisema ujenzi wa bandari hiyo utafungua fursa za kiuchumi katika mkoa wa Katavi, Rukwa, Kigoma na maeneo mengine yanayozunguka eneo hilo na taifa kwa ujumla.

Shaka alieleza ujenzi wa Bandari hiyo ambao sasa umefika zaidi ya asilimia 60, unaonyesha dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika na kuongeza vichocheo vya ukuaji wa uchumi.

error: Content is protected !!