CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza kuanza kutoa fomu za kuwania Uspika na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Pia, nafasi za Meya wa halmashauri ya jiji, manispaa na mwenyekiti wa halmashauri za wilaya nchini humo kuanzia leo Jumatatu hadi kesho Jumanne 3 Novemba 2020.
Muda huo wa siku mbili yaani leo na kesho ni sawa na saa 48.
Hatua hiyo inatokana na kuhitimishwa kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020 ambapo CCM kimejikusanyia wabunge wa majimbo zaidi ya 250 kati ya 265 na madiwani wengi zaidi.
Hii inaonyesha, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM itaongoza halmashauri karibu zote nchini humo ikiwa ni tofauti na hali ilivyokuwa mwaka 2015 ambapo vyama vya upinzani viliongoza Halmashauri 23 zikiwemo za majiji kama ya Dar es Salaam, Arusha na Mmbeya.

Katika Bunge la 11 lililomalizika, lilikuwa likiongozwa na Job Ndugai na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson.
Wote wawili, wamerejea bungeni, Ndugai alipita bila kupigwa Jimbo la Kongwa, Dodoma huku Dk. Tulia amemshinda Joseph Mbilinyi maarufu Sugu wa Chadema Jimbo la Mbeya Mjini.
Leo Jumatatu, tarehe 2 Novemba 2020, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametoa taarifa kwa umma akiwataka wanachama wa chama hicho wanaotaka kuwania nafasi hizo kujitokeza kuchukua fomu.
“Chama kinaalika wanawachama wenye sifa stahiki kwa mujibu wa sheria wanaoomba wafikiliwe na chama kwa nafasi ya Spika na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, meya wa halmashauri ya jiji au manispaa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya wajitokeze kuchukua fomu,” amesema Polepole
Polepole amesema, fomu za maombi ya nafasi ya Spika na Naibu Spika zitatolewa tarehe 2 hadi 3 Novemba 2020 katika Ofisi za CCM Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar.
“Kwa nafasi ya meya wa jiji au manispaa na mwenyekiti wa halmashauri fomu zinapatikana katika ofisi za CCM za wilaya,” amesema.
Polepole amemesa, tarehe 4 Novemba 2020 Kamati za Siasa za Wilaya za CCM zitajadili maombi ya waliojitokeza na kutoa mapendekezo tarehe 5 Novemba 2020 kamati za siasa za mikoa zikutane kujadili kisha zitoe mapendekezo.
“Mapendekezo ya kamati za siasa za wilaya na mikoa yawe yamefika ofisini kwa katibu mkuu wa CCM jijini Dodoma si zaidi ya saa 10:00 jioni tarehe 6 Novemba 2020,” amesema Polepole
Leave a comment