May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yataja sababu za kumsamehe Membe

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimemsamehe aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu yake Taifa (NEC), Benard Membe na Abdallah Diwani, kwa kuwa wamekiri makosa yao na kuomba radhi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Sababu hizo zimetajwa leo Ijumaa, tarehe 1 Aprili 2022 na Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Christina Mndeme, akihojiwa mbashara na kituo cha Televisheni cha Channel Ten, kuhusu maandalizi ya mkutano mkuu wa chama hicho, unaofanyika jijini Dodoma.

Mndeme amesema Membe na Diwani, waliomba msamaha na kutaka kurejea baada ya kuonja moto walipokwenda katika vyama vingine.

“Wajumbe wa NEC kwa kauli moja wamewasamehe sababu walikwisha fukuzwa uanachama, wameomba kurudishwa uanachama. Wamerudi wamekiri wamefanya makosa na wameona moto uliowawakia nje na wamerudi tunamshukuru Mungu kwa kutuongoza katika hili na wajumbe kwa pamoja wakawasamehe,” amesema Mndeme.

Katika hatua nyingine, Mndeme amewaomba wajumbe wa mkutano mkuu, kumpitisha Abdulrahman Kinana, katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, baada ya jana kupitishwa kugombea nafasi hiyo na NEC.

Membe alifukuzwa CCM Tarehe 28 Februari 2020, baada ya kukutwa na hatia kwa makosa ya utovu wa nidhamu kufuatia kuvuja kwa sauti yake iliyokuwa na mazungumzo yaliyodai CCM ilishindwa kuwalinda wastaafu wake dhidi ya watu wanaowachafua mitandaoni.

Baada ya Membe kutimuliwa CCM, alijiunga na Chama cha ACT-Wazalendo, ambapo chama hicho kilimpitisha kupeperusha bendera yake katika nafasi ya Urais wa Tanzania, kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Mapema Januari 2021, Membe alijivua uanachama wa ACT-Wazalendo.

error: Content is protected !!