May 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

CCM yapata msiba Z’bar

Marehemu Zawadi Salehe Makame

Spread the love

KADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Visiwani Zanzibar, Zawadi Salehe Makame, amefariki dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Radio ya Serikali ya Zanzibar, Zawadi amefikwa na mauti jana Jumanne, tarehe 17 Novemba 2020, katika hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja.

Hakuna taarifa zaidi ya kile alichokuwa kikimsumbua Zawadi na lini alipelekwa kwenye hospitali hiyo kwa matibabu.

Zawadi ambaye alikuwa mwanachama wa taasisi iliyopewa jina la Mimi na Mwinyi, anatarajiwa kuzikwa leo, kwenye makaburi ya Mwanakwelekwe, Unguja.

Mwanasiasa huyo alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na matamshi yake kizani, aliyekuwa akiyatoa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu uliyopita, yakiwamo yale yaliyodai kuwa “ushindi wa CCM, ni lazima.”

Akizungumza na viongozi wa matawi ya chama hicho, tarehe 3 Oktoba mwaka huu, Zawadi alisema, “…“nimekuja hapa kutaka tuzungumze kwa jinsi gani, mmejipanga kwenye uchaguzi huu. Hii ni kwa sababu,   ushindi wa CCM, hauna Mungu akipenda. Ushindi wa CCM, ni wa lazima.”

Aliongeza: “Hivi mnajua? Ushindi wa CCM siyo mpaka Mungu apende. Mungu akijalia. Aaaaa. Ushindi wa CCM, ni lazima. Ushindi wa CCM, ni lazima, hata iweje. Siyo kuwa Mungu akipenda. Kushinda ni lazima na hakuna Mungu akipenda.”

Matamshi haya ya kada huyo yalichukuliwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kidini, hasa waumini wa Kiislamu, kama yalivuka mipaka ya kampeni za kisiasa, na hivyo kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Ni kufuatia matamshi hayo na ubishani uliotokana na kauli hiyo, video ya kiongozi  huyo wa CCM, ilipata umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa kwenye makundi ya mtandao wa kijamii wa Whatsapp.

error: Content is protected !!