May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yamkingia kifua Rais Samia

Mgombea Urais wa CCM, John Magufuli (kushoto) akiwa na mgombea mwenza wake Samia Suluhu

Spread the love

 

CHAMA tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewatoa wasiwasi wanachama wake kwa ujumla kikisema mambo yatakwenda kama yalivyopangwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Mzee Phillip Mangula, leo Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, katika shughuli ya kitaifa ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

“Mambo yatakwenda, niwatoe wasiwasi wanachama na wananchi kwamba mambo yatakwenda kama yalivyopangwa,” amesema Mzee Mangula.

Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara)

Mangula amewatoa wasiwasi Watanzania kufuatia kifo cha Hayati Rais Magufuli, kilichotokea Jumatano tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Saalam.

Hayati Rais Magufuli amekuwa kiongozi wa kwanza kufariki akiwa madarakani. Ambapo alifariki dunia miezi minne, tangu alipoapishwa kuongoza muhula wake wa mwisho tarehe 5 Novemba 2020, baada ya kushinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akizungumzia tukio hilo la kihistoria, Mzee Mangula amesema, Rais wa Tanzania wa sasa, Samia Suluhu Hassani, ataendeleza yale yaliyoachwa na Hayati Rais Magufuli, kwani anayafahamu vyema kwa kuwa alikuwa msaidizi wake wa karibu.

“Hayati Rais Magufuli na Rais Samia walianza kwanza 2015, walizuguka wote nchi nzima wakichukua kitabu, safari hii kuna kitabu Ilani ya CCM ina kurasa 303 walisema kazi iliyo mbele yetu iko humu.”

“Naimaini kabisa baada ya zile ahadi, na kwa sababu walizunguka nchi nzima walikuwa wawili na walichukua benderea ya CCM wote, Rais Samia atafanya vizuri,” amesema Mzee Mangula.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais Samia alikuwa mgombea mwenza wa Hayati Rais Magufuli na kufanikiwa kushinda kiti cha Urais wa Tanzania, kisha wakaunda Serikali ya awamu ya tano.

Hadi umauti unamkuta Hayati Rais Magufuli, Rais Samia alikuwa makamu wake wa rais. Nafasi aliyohudumu tangu awamu ya kwanza ya kiongozi huyo hadi awamu yake mwisho ambayo mwanasiasa huyo aliiacha njiani baada ya kupoteza maisha.

Jeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli

Akizungumzia mabadiliko hayo ya uongozi, Mzee Mangula amesema, Rais Samia atafanya vizuri kama alivyomsaidia vyema Hayati Rais Magufuli enzi za utawala wake, hadi wakafanikiwa kushinda tena uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Bahati nzuri ile awamu ya kwanza walifanya vizuri sana na tathimini inaonesha kazi ilifanyika, hivi sasa hii ilani ya mwaka jana, walipita nchi nzima wakawaambia tuliyopanga kufanya kwa miaka mitano ijayo mpaka 2025,” amesema Mzee Mangula.

Mzee Mangula amesema “Bahati nzuri baada ya kumaliza ile kazi wananchi wakakubali kwa asilimia84.7, kwamba tunafiki hili.”

Mmoja wa waombolezaji akiwa katika hali ya simanzi mara baada ya Kuaga

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, Hayati Rais Magufuli alishinda kiti cha urais wa Tanzania baada ya kupata asilimia 84.7 ya kura. Ikiwa ni ongezeko la kura ikilinganishwa na alizopata katika uchaguzi wake wa mwanzo (2015).

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, mwanasiasa huyo alishinda kwa kupata kura asilimia 58.

Mzee Mangula ametoa matumaini hayo akisema, baadhi ya watu wana wasiwasi na hofu juu ya kifo cha Hayati Rais Magufuli.

“Maneno yaliyoelezwa hapo awali kwa ujumla wake, yanaonesha kuna simanzi kubwa, majonzi na masikitiko makubwa. Halafu kuna hofu na wasiwasi kwamba rais wetu tuliyemzoea ametutoka hatupo naye sasa itakuwaje?

Picha ya mjane Janeth Magufuli, akiaga mwili wa mume wake leo Dodoma

“Nataka tu nikumbushe kwamba, Rais Magufuli wakati huo na Samia ndiyo waliopita nchi nzima kueleza shabaha na makusudio ya chama chetu juu ya mambo ya kufanya nchi nzima katika miaka mitano ijayo,” amesema Mzee Mangula.

Hata hivyo, Mzee Mangula amesema, vikao vya Bunge lijalo, vitapitisha mpango wa
maendeleo ulioachwa na Hayati Rais Magufuli, ambao utatekelezwa na Rais Samia.

“Baada ya wananchi kukubali (kumpa ushindi Hayati Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana), serikali iliweka mpango wa namna ya kutekelea ahadi waliyopita kuzunguka na kueleza wananchi.

Baad ya serikali kuweka mpango wa maendeleo, ule mpango utakwenda kwenye bunge,” amesema Mzee Mangula na kuongeza:

“Nilikuwa namuulizia spika wa bunge (Job Ndugai) linakutana lini kujadili mpango wa maendeleo, akasema bunge hili litapitisha mpango wa maendeleo wa kazi zile zote, kwa hiyo msikate tamaa kazi zitafanyika.”

Mwili wa Hayati Rais Magufuli unatarajiwa kuzikwa Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, kijijini kwao Chato mkoani Geita.

error: Content is protected !!