June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Moyo: Sitapigania uanachama wangu CCM

Mwanasiasa Mkongwe nchini na muasissi wa siasa za maridhiano Zanzibar, Nassor Hassan Moyo

Spread the love

MWANASIASA mkongwe nchini na muasissi wa siasa za maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, ambaye jana alinyang’anywa uanachama wake katika Chama cha Mapinduzi (CCM) alichoshiriki kukianzisha 5 Februari 1977, amesema hatapigania uanachama wake huo. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Muda mfupi baada ya taarifa za kufukuzwa kwake na wajumbe wa Halmashauri ya Mkoa wa Mjini Magharibi, kupatikana na hatimaye kuthibitishhwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kupitia taarifa yake ya habari ya saa moja usiku, mzee Moyo alitamka kwamba hafikirii kukata rufaa.

“Siioni sababu ya msingi hata moja ya kukata rufaa ili tu niendelee kubaki CCM. Hawa wameshaonyesha kuwa hawanitaki, hawana shida namimi, wala hawajali kwamba mimi nimeshiriki kukianzisha chama hiki. Sasa sina sababu ya kupigania uanachama wangu CCM,” mzee Moyo alisema akizungumza na mwandishi wa MwanaHALISI Online.

Mzee Moyo amesema kwa njia ya simu kutoka nyumbani kwake jijini Tanga alikowasili juzi jioni, akitokea mjini Zanzibar, kuwa katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, amekuwa akisimamia misingi ya kulinda serikali ya umoja wa kitaifa (SUK), ambayo msingi wake ni siasa za maridhiano kwa Wazanzibari wote bila ya kujali itikadi zao kisiasa.

Mwanasiasa huyo ambaye asili ya baba yake ni Songea, mkoani Ruvuma, mwenyewe akiwa amezaliwa mjini Zanzibar, miaka 81 iliyopita, amekuwa na wake wawili, mmoja mjini Zanzibar na wa pili jijini Tanga. Amesema ratiba yake ya awali, anayodhani itabadilishwa kwa jambo la dharura tu, ni kukaa Tanga kwa mwezi mzima.

“Nitakaporudi nitakuwa na mkutano mkubwa kuzungumzia suala hili. Mimi naijua historia ya chama hiki wanachonifukuza. Naijua misingi yake na yale tuliyokubaliana kuyapigania. Wanavyoendesha mambo sasa hayapo katika malengo yale tuliyoweka,” anasema.

Ametoa kauli hii baada ya kujulishwa sababu za kufukuzwa CCM ikiwemo ya kuonekana mvunja maadili na miiko ya mwanachama. Katibu wa CCM Mkoa wa  Mjini Magharibi, Aziza Mapuri alisema katika taarifa iliyohusu uamuzi wa kufukuzwa kwa mzee Moyo, kwamba amekuwa akivunja miiko ya chama kwa kupanda kwenye majukwaa na kuhutubia mikutano inayoandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), anachojua ni hasimu wa CCM.

Taarifa ya Aziza imesema uamuzi uliochukuliwa dhidi ya mzee Moyo umezingatia nguvu za Ibara ya 93(14) ya Katiba ya CCM.  

ZBC iliyothibitisha uamuzi wa kufukuzwa mzee Moyo ilinukuu taarifa ya Aziza, akisema kuwa umetokana na maamuzi ya kikao cha Halmashauri ya Mkoa wa Mjini Magharibi kilichoketi kwenye Tawi la CCM Mbweni. (Awali tulitangaza kwa makosa kuwa kikao kilifanyika Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui mjini Zanzibar).”

Hatua ya kumfukuza Mzee Moyo inamaana Kamati ya Maridhiano iliyokuwa na wajumbe sita, watatu kutoka CCM na watatu kutoka CUF, ni shubiri kwa CCM ambayo baadhi ya viongozi wake wakuu wanataka serikali ya umoja wa kitaifa ivunjwe.

Waliokuwa na mzee Moyo kwenye Kamati ya Maridhiano ni Mansour Yussuf Himid ambaye alifukuzwa Agosti 2013 na Mohammed (Eddy) Riyami aliyejiondoa mara baada ya Mansour kufukuzwa uanachama na Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Wote sasa wanafanya kazi na CUF kusaidia kampeni ya kupatikana Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Mansour ambaye ameteuliwa kuwa Katibu wa kamati ya mkakati ya kuhakikisha ushindi wa Maalim Seif Sharrif Hamad, ameshatangaza kugombea uwakilishi jimbo la Kiembesamki.

Mapema jana, mzee Moyo aliiambia MwanaHALISI Online kuwa taarifa za kufukuzwa alizisikia juu juu tu, kwani hajapewa taarifa rasmi. Mpaka jioni hii hakuarifiwa rasmi kuhusu uamuzi huo.

“Mimi sipo Zanzibar, taarifa hizo nimezisikia juu juu tu, lakini muda muafaka ukifika nitatoa tamko rasmi,” anasema Mzee Moyo anayemiliki kadi namba saba.

Mzee Moyo anasema, hashangai kusikia kuwa amefukuzwa kwani mara kadhaa viongozi wa CCM wa mkoa wa Wilaya, walikuwa wanamtaka awarushie kadi yake ya uanachama, lakini aligoma na kuwaambia labda akiitaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

Fukuto la kushinikiza kuvuliwa uanachama mzee Moyo, lilianza tangu kamati yake ya Maridhiano ilipofanikisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa baada uchaguzi 2010 ambapo amekuwa akipigania kuwepo Muungano wa serikali tatu anaosema ndio wa haki na ambao utaipa Zanzibar serikali yenye mamlaka kamili, kinyume na ilivyo uhai wote wa Muungano miaka zaidi ya hamsini.

Msimamo huu unapingana na sera ya CCM inayoshikilia Muungano wa Serikali mbili. Msimamo wake unachukuliwa kama ni msimamo unaoendana na CUF hivyo kuwekwa kundi la kusaliti CCM.

error: Content is protected !!