Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CCM ‘yalia’ hujuma, yaipa rungu Takukuru
Habari za SiasaTangulizi

CCM ‘yalia’ hujuma, yaipa rungu Takukuru

Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM
Spread the love

 

WAKATI hali ya upatikanaji maji ikizidi kuwa tete katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania, chama tawala nchini humo- Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimedai kuwapo hujuma za kukwamisha ujenzi wa miradi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Madai ya CCM kuhusu hujuma kwenye miradi ya maji, imekuja siku chache kupita tangu Rais Samia Suluhu Hassan, kuwatangazia vita wanaohujumu miundombonu ya vyanzo vya maji na kusababisha adha kubwa kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akiwa katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bugando yaliyofanyika Mwanza, Rais Samia alitaja mambo manne yanayosababisha tatizo la maji nchini.

Alitaja mambo hayo ni pamoja na tabia ya kunywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji, watu kuchepusha maji kutoka mitoni kwa ajili ya kilimo, ukataji miti katika vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema juzi kuwa chama hicho kimedai kimeshitushwa na hatua ya baadhi ya wakandarasi kujitoa kwenye miradi mikubwa ya maji, bila kueleza sababu na bila kujali kwamba walishasaini na kuanza kazi ya upembezi yakinifu.

Juma Aweso, Waziri wa Maji

Kutokana na hali hiyo, chama hicho tawala kimeiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchunguza kujitoa kwa wakandarasi wa maji nchini, katika mazingira tatanishi.

Mmoja wa wakandarasi anayelalamikiwa kujitoa ghafla kwenye ujenzi wa mradi mkubwa wa majini ni kampuni ya Spencon Service, ambayo ilijitoa katika hatua za mwanzo za ujenzi wa mradi wa maji wa Ziwa Tanganyika.

“Sisi kama chama, tuna imani kubwa na nyie watendaji mliopewa dhamana ya kusimamia na jitihada hizi mnazofanya, lakini sasa mnahitaji kuongeza umakini na uzalendo.”

“Kwani mnaweza kuwa makini, lakini uzalendo hamna, yapo baadhi ya maeneo hadi wakandarasi wanajitoa, kuna mambo mengi nyuma yake,” alisisitiza.

“Hapa sasa ni mtu mmoja keshajitoa na huyu aliyepo sasa ni wa pili, hii ni shida kubwa ya wakandarasi kuondoka katika mazingira kwa utata kiasi hiki,” alisema.

Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

Kwa mujibu wa Shaka, juzi alizungumza na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhusu tatizo la wakandarasi kujitoa, ambaye alimwambia kuwa hivi karibuni anakusudia kukutana na wakandarasi wa ujenzi wa miradi ya maji nchi nzima kuzungumzia changamoto hiyo.

“Sisi tunawapa kazi, wakandarasi wetu tunawaamini ila sasa wanaturudisha nyuma maana kila siku tunaimba tatizo la maji ukija huku unakuta mkandarasi kajitoa,” alisema Shaka.

Chama hicho, kimesisitiza ni vema uchunguzi huo wa Takukuru ukaanzia ndani ya Wizara ya Maji, ili kujua sababu inayofanya wakandarasi hao kuondoka na kuacha miradi kabla ya kukamilika au ujenzi kuanza.

Shaka alisema hivi sasa jicho la CCM, litakuwa katika mradi wa maji wa Ziwa Tanganyika, kuona namna gani utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia, unafanyika kwa uhakika ili wananchi wapate huduma hiyo.

Akizungumza alipotembelea mradi huo unaotekelezwa katika kata ya Bangwe, Kigoma Ujiji, Shaka alisema njia pekee ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama, ni kwa mikoa iliyo karibu na maziwa, kuhakikisha Serikali inakamilisha miradi mikubwa iliyojipangia.

Alisema ni jukumu la msingi kwa Wizara ya Maji hususan kwa ofisi zilizo kwenye mikoa yenye maziwa, kuhakikisha wanapunguza au kutatua changamoto zilizopo.

“Wizara ya Maji hili ni jukumu lenu la msingi, hususan nyie mlioko ziwani, tunataka tutoke huku sasa, sababu kimbilio pekee la kupunguza au kutatua changamoto ya maji, ni kutumia rasilimali hii ya Ziwa,” alisema Shaka.

Hata hivyo, Shaka hakutaja wakandarasi wengine waliojitoa kwenye ujenzi wa miradi ya maji.

Salumu Hamduni mkurugezni mkuu wa TAKUKURU

Hivi sasa, mradi wa Ziwa Tanganyika, unatekelezwa na kampuni ya Sino Hydro Corporation katika maji ya Ziwa hilo, kwa ajili ya ujenzi wa kitekeo kipya cha maji katika eneo la Amani Beach.
Mkurugenzi KUWASA

Awali, akiwasilisha taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (Kuwasa), Mbike Jones, alisema mradi za Ziwa Tanganyika, unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji.

Wizara imeingia mkataba na mkandarasi, Sino Hydro Corporation, kwa ajili ya ujenzi wa kitekeo kipya cha maji eneo la Amani Beach.

Alisema mradi huo ulitiwa saini Novemba 23 mwaka jana na kuanza kazi Julai 19 mwaka huu, ukiwa chini ya wizara hiyo na umefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW).

Alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika Julai 19 mwakani, ambapo shughuli zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji yasiyosafishwa chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 42 za maji kwa siku.

Pia, ujenzi wa bwawa la muda ili kuwezesha ulazaji bomba la kipenyo cha milimeta 1,000 la kuchukulia maji kutoka Ziwa Tanganyika.

Shughuli zingine, ni ujenzi wa kambi ya mkandarasi, barabara ya muda kwa ajili ya kusafirisha vifaa na mitambo ya mkandarasi, kufika eneo la kitekeo kipya cha maji na uhamishaji wa pampu za maji yasiyosafishwa.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda, alisema mradi huu ni kama kitendawili kwa wananchi, kwani umechukua muda mrefu bila kukamilika.

Alisema kukamilika kwa mradi huo, kutaleta ahueni kwa wananchi na hadi sasa wanapata Sh milioni 500 kutoka fedha za Uviko-19 walizopewa na Serikali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!