Spread the love

 

CHAMA tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimejinasibu katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara, kimefanikiwa kuenzi mfumo wa vyama vingi na ugatuaji wa madaraka kwa amani. Anaripti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mafanikio hayo yametajwa leo Jumatano, tarehe 8 Desemba 2021 na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, akitaja mafanikio ya nchi tangu Tanzania Bara ilipopata uhuru wake tarehe 9 Desemba 1961.

Chongolo amesema, tangu nchi ishikiliwe na vyama vianzilishi vya CCM, Tanu na ASP, chama hicho tawala kimefanikiwa kusimamia na kuiongoza nchi katika mabadiliko ya mfumo wa vyama vingi.

“Nafikiri mmenielewa kwamba katika miaka 60 ya uhuru, moja ya mafanikio ya chama chetu ni kusimamia mchakato wa kuruhusu maoni ya wachache waliotaka mfumo wa vyama vingi nchini kuchukua nafasi na kutekelezwa na kututoa kwenye chama kimoja kwenda kwenye vyama vingi,” amesema Chongolo.

Katibu mkuu huyo wa CCM, amesema chama chake kimefanikiwa kuondoa mfumo wa chama dola.

“Wapo ambao wako ‘busy’ kubeza, lakini hayo ni mafanikio ya muhimu na makubwa kwa nchi kwani duniani ni nchi chache sana zimevuka na kuendelea kuwa na vyama vinavyoongoza nchi, ambavyo vimeratibu na kusimamia mageuzi makubwa ya kimfumo kama haya,” amesema Chongolo.

Chongolo amesema “kumbuka mwanzo tulikuwa ni chama dola, tulikuwa na wakuu wa wilaya ambao walikuwa makatibu wa wilaya kwenye maeneo yao, tulikuwa na wakuu wa mikoa ambao pia walikuwa makatibu wa mikoa kwenye maeneo yao.”

Mwanasiasa huyo amesema, CCM inaendelea kutenganisha mfumo wa chama na Serikali.

“Tunakwenda kutengenisha mfumo wa kuwa Serikali chama, au chama Serikali au chama dola, tunaruhusu mchakato urudi kwenye utaratibu wa kukaa pembeni na kuongoza ukiwa pembeni na baadae unaendelea kuaminiwa na wananchi unaongzoa nchi mpaka leo sio jambo dogo nikubwa sana,” amesema Chongolo.

Wakati huo huo, Chongolo amesema CCM imefanikiwa kuongoza mabadiliko ya mfumo wa sheria na katiba.

“Tumefanikiwa kusimamia na kuongoza mchakato wa mabadiliko ya sheria mbalimbali na katiba ya nchi kwa kadri ya mahitaji ya nyakati tofauti, kuanzisha na kuimarisha vyombo mbalimbali vya kusimamia utawala bora,” amesema Chongolo.

Mafanikio mengine yaliyotajwa na Chongolo, ni nchi kubadilisha uongozi kwa amani kupitia sanduku la kura, na kuifanya Tanzania kuwa mwalimu wa demokrasia kwani hakuna kiongozi aliyejiongezea madaraka.

“Tanzania imekuwa mwalimu wa demokrasia kwani hakuna kiongozi hata mmoja aliyediriki kujenga tamaa binafsi na kufikiria kubadilisha katiba ili ajiongezee dhamana au muda au muhula wa kuongoza nchi, hili ni jambo kubwa la kupigiwa mstari na hiyo ndiyo demokrasia ya kweli,” amesema Chongolo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *