January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yajianika itashinda 69%

Spread the love

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) chenye historia ya woga kuruhusu wagombea wake kushiriki majadiliano ya wazi, kimejitokeza kuwa tayari mgombea wake wa urais wa jamhuri, Dk. John Magufuli, ashiriki. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Katika mshabaha huohuo wa kujianika, kimejitangazia ushindi wa zaidi ya asilimia 69 wakati kinakiri katika tamko lake la jana, kuwa mgombea huyo amefikia asilimia 30 tu ya wapigakura. Zaidi ya watu 23 milioni wameandikishwa kupigakura Oktoba 25 mwaka huu.

Jumanne wiki hii, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), James Mbatia alitangaza kuwa umoja huo unafuatilia kwa karibu mipango michafu inayofanywa na CCM ya kusaka ushindi wa hila.

Ukawa unaundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD) waliofanikiwa kuweka mgombea mmoja wa urais ambaye ni waziri mkuu aliyejiuzulu 2008, Edward Lowassa.

Mbatia amesema umma umedhihirisha kutaka mabadiliko ya uongozi kwa kumuunga mkono Lowassa aliyehama CCM Agosti 28 akitafuta njia ya kutimiza dhamira yake ya kuongoza taifa baada ya kuhujumiwa na CCM.

Katika tamko lililotolewa jana na CCM kupitia mjumbe wake wa kamati ya kampeni, January Makamba, imeelezwa wagombea wao watashiriki.

Tena, chama hicho kimeshangaa msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), uliotolewa na Mwenyekiti mwenza, James Mbatia, kwamba wangependa wakuu wa vyama ndiuo washiriki na sio wagombea.

Mbatia alisema Jumanne wiki hii kuwa viongozi wa vyama ndio wanaostahili kushiriki midahalo kwa kuwa ndio wanaowasimamia wagombea.

Lakini Makamba ambaye alisoma tamko la CCM mbele ya waandishi wa habari, amesema “CCM inaamini kwamba ili mdahalo huu uwe na tija, wagombea urais wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki.”

Chama hicho kinasema mdahalo unapaswa kuwa baina ya wagombea kwa kuwa “wao ndio wanaoomba dhamana… wanapaswa kujibu maswali na kufafanua kuhusu ahadi zao.”

Mara kadhaa katika uchaguzi uliopita, CCM imezuia wagombea wake akiwemo wa urais, kushiriki mdahalo, bila ya kutoa sababu ya msingi.

Katika hatua nyingine, tamko la CCM kupitia Makamba ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), linasema kwa tahmini waliyoifanya, mgombea Magufuli tayari ana asilimia 69.3 ya kura zitakazopigwa katika uchaguzi wa Oktoba 25.

Makamba amesema kufikia Septemba 16, jana, mgombea ameshafikia asilimia 30 ya wapigakura nchini, kutokana na mikutano 76 ya hadhara na mikutano mingine 381 ya “barabarani.”

Dk. Magufuli ameshatembelea mikoa 12 na majimbo 94 katika safari hiyo ya kampeni iliyoanza rasmi Agosti 23, mwaka huu.

Chama hicho kimesema kinasikitishwa na ilichosema “kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa UKAWA zenye kuashiria fujo na vurugu.” Tamko limetaja kauli ya hofu ya umoja huo kuibiwa kura, bali amesema haina msingi.

“Utaratibu wa uchaguzi wetu unajulikana na umekubalika na vyama vyote. Kura zinapigwa kituoni na kuhesabiwa kituoni mbele ya mawakala wa vyama vyote, wasimamizi wa uchaguzi na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi,” amesema Makamba ambaye anagombea tena ubunge jimboni Bumbuli ambako tayari alijaribu kulazimisha ushindi kwa kujitangazia kuwa hana mpinzani.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima ilikataa pingamizi aliyowekewa mgombea wa UKAWA jimboni Bumbuli.

error: Content is protected !!