May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yaitisha kamati kuu

Humphrey Polepole, Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

Spread the love

 

CHAMA tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeitisha kikao cha dharula cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wake, Dk. John Pombe Magufuli, kilichotokea jana Jumatano tarehe 17 Machi 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi tarehe 18 Machi 2021 na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole wakati anazungumza na wanahabari kuhusu msiba huo mzito, Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dodoma.

Polepole amesema, kikao hicho cha dharula kimeitishwa na Makamu wenyeviti wa chama hicho, Mzee Phillip Mangula (Bara) na Rais Mastaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (Zanzibar).

Na kitafanyika Jumamosi tarehe 20 Machi 2021 majira ya saa 8.00 mchana kwenye ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

“Wakuu wa chama waliopo, Mzee Mangula na Mzee Shein wameshauriana na kukubaliana, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa iketi kwa kikao maalumu siku ya Jumamosi katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Lumumba,” amesema Polepole.

Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara)

Sambamba na hilo, Polepole amesema chama hicho kitasimamisha shughuli zake kwa muda usiojulikana pamoja na kuombeleza kwa muda wa siku 21.

“Kama mnavyofahamu Rais Magufuli amekuwa mwenyekiti wa CCM kutoka 2016 mpaka umauti ulipomfika na amekuwa Rais wa Tanzania kutoka 2015 hadi umauti ulipomfika. Chama kitaomboleza kwa siku 21,” amesema Polepole na kuongeza:

“Kutakuwa na kitabu cha maomboleza katika ofisi kuu za chama, Dodoma, Dar es Salaam na Kisiwandui Zanzibar.”

Dk. Bashiru aliapishwa siku iliyofuata yaani 27 Februari 2021, Ikulu ya Dar es Salaam, akichukua nafasi iliyoachwa na Balozi John Kijazi, ambaye alifariki dunia tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.

Akitangaza kifo cha Hayati Rais Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassani, alisema kiongozi huyo alifariki dunia katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Mama Samia anayesubili kuapishwa ili kuwa Rais kumalizia muda uliobaki wa miaka takribani minne, alitangaza siku 14 za maombolezo na bendera zitapepea nusu mlingoti.

Rais Magufuli aliingia madarakani kuongoza Serikali ya awamu ya tano tarehe 5 Novemba 2015 baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu.

Alifanikiwa kumaliza muhula wake wa kwanza wa awamu hiyo, hadi aliposhiriki tena Uchaguzi Mkuu wa 2020, na kufanikiwa kushinda tena uchaguzi huo na kuendelea na awamu ya pili wa uongozi wake, hadi umauti ulipomkuta, akiwa ametumikia kwa takribani miezi minne kwenye ungwe ya miaka mitano ya pili.

Rais Magufuli alikuwa Mwenyekiti wa CCM kuanzia 2016 hadi umauti ulipomkuta mwezi Machi, 2021.

error: Content is protected !!