December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

CCM yaitaka HESLB kutoa kipaumbele kwa watoto masikini

Spread the love

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeielekeza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kuendelea kutoa kipaumbele kwa kundi la watoto masikini na wenye mahitaji maalumu wenye vigezo vya kunufaika. Anaripoti Mwandishi wetu…(endelea)

Pia, kimeipongeza bodi hiyo kwa kazi nzuri inayoifanya ya kuwafikia wanafunzi, huku ikisema ongezeko la marejesho ya mikopo kutoka kwa wanufaika kulikotokana na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kufuta Kodi ya ongezeko la zuio kwenye Mikopo ya elimu ya Juu (Retention fee), ni kielelezo cha ufanisi.

Hayo ameelezwea leo tarehe 26 Oktoba, 2021 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alipotembelea HESLB kuona jinsi inavyofanya kazi.

Amesema ni lazima kundi la watoto masikini na wenye mahitaji maalumu lipewe kipaumbele zaidi na kuhakikisha hakuna mwanafunzi yeyote aliyekidhi vigezo vya bodi anakosa mkopo.

Amesema Ilani ya  Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ibara ya 80 (h) inasema serikali itaimarisha na kuboresha mfumo wa ugharimiaji wa elimu ya juu ikiwemo bodi ya mikopo ya Juu, ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji na sifa stahiki wanapata fursa ya kujiunga na elimu ya juu.

Amesema Rais Samia ameonyesha dhamira ya dhati kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa ya kusoma ambapo, ameongeza mkopo wa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka sh bilioni 464 hadi sh. bilioni 570.

“Tunaona na kutambua kazi nzuri inayoifanya na Bodi ya Mikopo, endeleeni kuchapa kazi. Ni jukumu la vijana wetu na Watanzania kwa jumla kutambua taratibu na kuzifuata ili kuepuka changamoto ndogondogo zinazojitokeza katika kufanikisha utoaji huduma.

“Msisitizo wetu wanafunzi wote wenye uhitaji na sifa  stahiki wa vyuo vyote viwe vya serikali ama  binafsi wapewe mkopo tena kwa wakati na haraka, bahati nzuri tumekuwa mfano katika Afrika katika kusimamia jambo hili la mikopo, hivyo liendee kufanyika kwa weledi ili kuondoa malalamiko,” ameshauri Shaka.

 Amesema kujitokeza kwa nchi za Uganda, Namibia, Rwanda na Zambia kuja kujifunza HESLB juu ya utoaji mikopo,  ni kielelezo cha uimara wa Tanzania katika jambo hilo na linapaswa kuendelea kusimamiwa vyema

“CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha sekta ya elimu nchini ikiwemo elimu ya Juu.

Aidha, akizungumzia kuhusu ongezeko la bajeti ya mikopo, Shaka amesema “Rais Samia kwa kuthamini kada hii ya elimu,  katika  kipindi kifupi ameongeza  bajeti ya mikopo nchini kutoka sh. bilioni 420 mwaka 2020/2021 hadi sh. bilioni 570 mwaka 2021/2022 ambapo wanafunzi wa mwaka wa kwanza takribani 70,000 watapata mikopo na wanaondelea na masomo 98,000 wanaendelea kunufaika na mkopo huu.”

Amesema pamoja na ongezeko hilo la fedha, Chama kinaendelea kusisitiza bodi ya mikopo kuendelea kupokea maoni na michango mbalimbali ya wadau wa elimu na kuyawasilisha serikalini ili kuendelea kuboresha zaidi mikopo inayotolewa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa HESLB, Veronica Nyahende amesema kazi ya kutoa mikopo katika mwaka wa masomo 2021/2022 inaendelea vizuri.

Amesema hadi jana walikuwa wameshatoa mikopo kwa asilimia 82 ya sawa na idadi ya wanufaika 60,356.

“Oktoba 28, mwaka huu tutatoa ‘bachi’ nyingine ya mikopo,” amesema.

Akizungumza kuhusu hali ya urejeshaji wa mikopo amesema ni nzuri na kwamba katika robo ya kwanza wamefanikiwa kukusanya Sh. bilioni 52 badala ya Sh. bilioni 45 iliyokuwa imekusudiwa awali.

Hilo limetokana na mwamko wa wanufaika hasa baada ya Rais Samia kufuta kodi ya ongezeko la zuio kwenye mikopo ya elimu ya juu (Retention fee).

error: Content is protected !!