Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CCM yahakiki madeni ya kampeni 2020
Habari za SiasaTangulizi

CCM yahakiki madeni ya kampeni 2020

Katibu wa Itikadi na uenezi CCM, Shaka Hamidu Shaka
Spread the love

 

CHAMA tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema, kinafanyia uhakiki madeni ya wafanyabiashara saba waliosema wanakidai, kutokana na kazi kiliyowapa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika taarifa ya CCM iliyosainiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka jana Alhamisi tarehe 28 Aprili 2022 na kusambazwa kwa vyombo vya habari, CCM ilisema inatambua madeni hayo kwa kampuni yake ya Uhuru Media Group (UMG).

“Kutokana na kutambua hilo, tayari chama kimeshachukua hatua mbalimbali zikiwamo zinazoendelea sasa za kufanya uhakiki ili kujiridhisha uhalali wake, kabla ya kuendelea na mchakato mwingine, baada ya kujiridhisha,” ilisema taarifa.

Jumla ya kampuni saba zilidai Jumanne wiki hii, kwamba zinadai Sh bilioni moja kutoka UMG, ambayo ni malipo na malimbikizo ya madai yao, baada ya kutoa huduma za kutengeneza na kusambaza sare na mabango wakati wa kampeni hizo.

Kampuni hizo saba za uchapishaji za Kariakoo, Dar es Salaam, zilitishia kuipeleka CCM mahakamani zisipolipwa fedha hizo.

Kampuni zinazoidai CCM ni FRT Printers, Master Samon Digital Print, Total Graphics Solution, Swab Trading Company, Mas General Supply, Mwamakula Production na Print Plus Limited.

Zilimwomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kuzisaidia kupata haki yao.

Mkurugenzi wa Total Graphics, Salum Mussa, aliomba walipwe fedha zao na kama maombi yao hayatafanyiwa kazi, watachukua hatua ya kwenda mahakamani.

“Haki haibembelezwi, sisi tunachotaka ni fedha zetu tulipwe, ni nyingi kwetu, zimetuingiza katika madeni kiasi kwamba huko mitaani tumeonekana matapeli.

“Kwa hali tuliyonayo sisi, hatuwezi kurejesha zimekuwa nyingi kutokana na riba kuongezeka,” alidai Mussa na kuongeza:

Elifadhar Mdassa, wa Master Samon Digital Print, alisema wameamua kutoka hadharani kudai malipo hayo, baada ya jitihada zao za kutafuta suluhu na UMG na uongozi wa CCM, kugonga mwamba.

Alisema, waliwahi kuzungumza na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa UMG, Ernest Sungura, lakini hakutatua tatizo lao.

Makamu Mwenyekiti wa chama tawala Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana

Mdassa alisema kila walipowasilisha malalamiko yao waliambiwa hayajafanyiwa kazi, kutokana na sababu mbalimbali, yakiwamo mabadiliko ya uongozi wa CCM na UMG, yaliyotokana na kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, Rais Dk John Magufuli.

“Tumefanya jitihada kubwa, mbali na kuonana nao ana kwa ana na kuandika barua kudai malipo yetu, lakini hazijazaa matunda, tukiambiwa kuna mabadiliko ya hapa na pale,” alisema Mdassa na kuongeza:
“Mara kukawa na msiba wa Rais, ngoja mtalipwa, muda unazidi kwenda ahadi tunazopewa hazikidhi matakwa yetu. Kimsingi wavae viatu vyetu waone hali tunayopitia, ni ngumu.”

Eliatosha Muganyizi, Mkurugenzi wa FRT Printers, alisema kampuni hizo ziliingia mkataba na UMG, Juni 2020, ili kutoa huduma za sare za CCM katika uchaguzi huo.

Muganyizi alisema kwa mujibu wa mkataba kati ya kampuni hizo na UMG, walipaswa kulipwa fedha zao ndani ya siku 30 baada ya huduma, lakini hadi leo baadhi ya kampuni zimelipwa nusu huku zingine zikikosa kabisa.

“Kuanzia Juni 2020 tulisambaza sare zikiwamo fulana, nembo za chama na vibeba funguo. Tulisambaza kwa miezi mitatu hadi uchaguzi ulipokwisha.

“Mimi kampuni yangu inadai Sh milioni 38 ambapo pamoja na ongezeko la riba ni Sh milioni 150, hadi sasa sijalipwa naomba nilipwe,” aliomba Muganyizi.

Elia Mwangayo, alisema: “Hadi leo tumefanya kazi ya chama chetu pendwa lakini hatujalipwa. Sisi hatuna ugomvi na chama chetu, ila tumeamua kuongea, baada ya kuona malalamiko yetu hayafanywi kazi.

Mwangayo alisema kutolipwa fedha hizo kumewaletea athari mbaya, ikiwamo baadhi yao kuuza mali kulipa madeni, huku mwingine aliyemtaja kwa jina la Fredy Mwamakula, akifariki dunia kutokana na msongo wa mawazo.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!