July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yadhihirisha ZAN-ID mtaji

Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shain

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimethibitisha kunufaika na utaratibu wa kuhusisha haki ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na maslahi ya kisiasa baada ya wawakilishi wake wote kushikamana na kuikataa hoja binafsi ya kuibana serikali kutenda haki kwa kuhakikisha kila mwenye haki anapewa kitambulisho hicho.

Wawakilishi hao katika Baraza la Wawakilishi walikataa hoja hiyo iliyowasilishwa mapema wiki hii na Mwakilishi wa jimbo la Ole, kisiwani Pemba, Hamad Masoud Hamad, anayetoka Chama cha Wananchi (CUF).

Hamad, aliyejiuzulu uwaziri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka juzi, alisema wakati wa kuwasilisha hoja yake hiyo kuwa kuna mtandao uliotengenezwa kwa makusudi ili kuzuia watu kupatiwa kitambulisho hicho kwa maslahi ya CCM.

Mhandisi huyo wa mitambo ya maji, alisema mtandao huo umetokana na shinikizo la CCM kutaka serikali ichague watu wa kupatiwa kitambulisho hicho, mbinu iliyolenga kuwanyima wale wanaoaminika, hata kwa hisia tu, si watiifu kwa CCM.

Alisihi wawakilishi wamuunge mkono na kupendekeza serikali itoe ufafanuzi wa sababu za kuwepo watu wengi wanaoendelea kulalamika kunyimwa kitambulisho hicho huku wakiwataja masheha na Idara ya Usajili wa Kitambulisho kama kikwazo cha haki hiyo.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya uongozi wa Amani Abeid Karume aliyestaafu urais baada ya miaka kumi mwaka 2010, ilipeleka barazani muswada na hatimaye ikatungwa sheria ya kuanzisha kutoa kitambulisho kwa kila Mzanzibari.

Muswada huo wa 2004, ulipingwa na wajumbe wa CUF kwa maelezo kuwa utatumika vibaya kukidhi malengo ya kisiasa kwa nia ya kuwazuia wananchi haki ya kushiriki uchaguzi wa kupata viongozi wao wa kisiasa – rais, wawakilishi na madiwani.

Hata hivyo, jitihada za wawakilishi wa CUF ambao ndio pekee watokao kambi ya upinzani katika baraza hilo, ziligonga mwamba baada ya CCM kutumia wingi wa wawakilishi wake kupitisha kwa kura.

Serikali harakaharaka iliunda Kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo kwa matarajio ya kitambulisho hicho kuhusishwa na masuala ya uchaguzi wa mwaka 2005. Taratibu ziliendelea licha ya upinzani mkubwa kutoka CUF.

Lakini hatimaye, mpango wa serikali ya CCM kutumia kitambulisho hicho katika uchaguzi uliofuata Oktoba 2005, ulikwama pale Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilipokataa kukitumia kitambulisho hicho kama sharti la mwananchi kuandikishwa kuwa mpigakura.

Njama za serikali ya CCM zilifanikiwa baadaye, na Tume ikaridhia kitambulisho hicho kuwa sharti mahsusi kwa kila anayetaka kuwa mpigakura kwa ajili ya uchaguzi wa Zanzibar ambao ndio kisheria unaosimamiwa na ZEC.

Utaratibu huo ulianza rasmi kukaribia uchaguzi mkuu wa 2010. Tume iliandikisha wapigakura upya kwa kutumia sharti hilo, huku sheria ya kitambulisho ikishurutisha kuwa mtu atahesabiwa kuwa mkaazi wa kudumu wa jimbo akiwa ametimiza miaka mitatu mfululizo kuishi hapo.

Kipengele hicho cha sharti la muda kilikwamisha haki ya kitambulisho kwa maelfu ya wananchi waliohamia Unguja kutoka kisiwa cha Pemba na hivyo kuachwa nje ya daftari la wapigakura la Zanzibar.

Hata pale mtu alipothibitisha kuwa ameishi ndani ya jimbo kwa kipindi hicho, serikali ilipenyeza sharti lisilo rasmi la mtu kuwa na cheti cha kuzaliwa ndipo apate kitambulisho.

Mbinu hiyo pamoja na vikwazo vinavyotokana na utumishi wa Masheha, viongozi wa mitaa, imeleta usumbufu mkubwa kwa umma wa wananchi, kwa kuwa sasa imethibitika kuwa hata wale waliomudu kuvuka vizingiti, wamekuwa wakinyimwa kitambulisho pamoja na kuwa wamesajiliwa na risiti ya kulipia wanayo.

Hayo ni mambo ambayo yamejumuishwa katika hoja binafsi ya Hamad Masoud Hamad, ambaye hatimae alipokuwa akifanya majumuisho ya hoja, baada ya majadiliano makali barazani, alitaka baraza liridhie kuibana serikali isimamie kupatikana kwa haki ya kitambulisho bila ya vikwazo.

Baraza lilielezwa kwamba kitambulisho hicho kimekuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi, kwa kuwa kinatakiwa kwenye maeneo mengi kama vile mtu anapotaka tiketi ya usafiri wa baharini na anga, pasipoti, leseni ya biashara na udereva pamoja na huduma ya umeme, maji na laini za simu za mkononi.

Hoja hizo hazikuwa za msingi kwa wawakilishi wote wa CCM waliochangia mjadala wa hoja hiyo Jumatatu wiki hii. Walisema hoja hiyo ilikuwa ya kisiasa, iliyowasilishwa kwa malengo ya kisiasa kwa vile suala hilo ni la muda mrefu.

Kwa mfano, Mwakilishi wa Kwamtipura, Unguja, Hamza Hassan Juma yeye alizidisha dharau kwa kuthubutu kuuchana waraka wa hoja hiyo alipomaliza tu kutoa mchango wake.

Alisema, “Hoja hii imekosa msingi na nguvu ya hoja, imejaa taswira ya kisiasa na propaganda; Baraza lisikubali vyombo vingine vivunje sheria. Kama kukosa ZAN-ID ni mtaji wa kushinda na kushindwa, CCM haina jimbo hata moja kisiwani Pemba.”

Machano Othman Said (Chumbuni) ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi (MBLM), alisema wapo watu wengi jimboni kwake waliolazimisha kuandikishwa wakati si wakazi halali na alipofuatilia alibaini ni kweli si wakazi halali.

Naye Ali Salum Ali (Kwahani) alisema anashangaa hoja hiyo kuletwa wakati huu (kuelekea uchaguzi mkuu), na kuhoji kwa muda wote wa malalamiko ya wananchi mletaji alikuwa wapi?

Mjadala wa hoja hiyo ulifungwa Jumanne baada ya mawaziri watatu wa SMZ kupinga hoja hiyo wakieleza kuwa hoja imejaa mtizamo wa kisiasa na imeondoka katika ukweli wa hali halisi kuwa serikali imekuwa makini katika kuhakikisha yule tu mwenye sifa ndiye anapatiwa kitambulisho na kwamba inavyo vitambulisho vingi havijachukuliwa na wenyewe.

Pia walitaka wananchi wafuate sheria iliyopo ya anayekataliwa na sheha kupanda ngazi ya juu kwa Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, na akikosa haki aende mahakamani ambako ni chombo cha kutoa haki kwa mwananchi anayekosa kwengineko.

Mawaziri hao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini (Dimani), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed (Wawi) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheri.

Mawaziri wote hao ni kutoka CCM, chama ambacho kinatumia nguvu zake za kudhibiti mamlaka ya uongozi wa serikali, licha ya kuwa ya ushirikiano pamoja na CUF kwenye ngazi ya mawaziri – hivyo wamejidhihirisha hata katika hoja zao kuwa wanakibeba chama hicho kwa maslahi ya kisiasa.

Waziri Aboud aliliambia baraza: “Kila mwananchi ana haki ya kupata kitambulisho bila kupuuzwa, ikitokea Mkurugenzi wa (Idara ya) Usajili wa Kitambulisho au Waziri anashindwa kiutimiza jambo hilo, mtu ana haki ya kwenda mahakamani.”

Hoja hiyo imeelezwa na wachambuzi kama kitendawili kwa kuwa ni dhahiri njia ya mahakama haiwezi kuwa ufumbuzi kwa vile si rahisi kila mwananchi kuweza kumudu.

Upo ushahidi wa maelfu ya watu waliofungua kesi mahakamani kudai kuandikishwa kuwa wapigakura, na kushinda kesi zao, hawakuandikishwa na Tume ya Uchaguzi, hali iliyothibitisha mtandao wa kunyima kitambulisho wanaoonekana kupendelea upinzani, umezama ndani ya Tume.

error: Content is protected !!