July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM yaanza kuporomoka

Wanachama wa Chadema wakiwa katika mkutano wao

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimejiandikia historia yake mpya ya kisiasa. Kimeangusha kwa kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi wa marudio wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika katika kata tatu za Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Uchaguzi wilayani Sumbawanga uliamriwa kurudiwa kutokana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu wa tarehe 14 Desemba 2014.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Hamid Njovu, kati ya mitaa 43, Chadema walishinda viti 37 na CCM waliambulia viti vitano tu.

Kata zilizorudia uchaguzi huo ni Msua, Chanji na Kizwite na mitaa miwili ambayo pia uchaguzi wake ulivurugika awali.

Njovu alisema uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti katika mtaa mmoja wa Nankasi, Kata ya Chanji, utarudiwa Jumapili baada ya kura kugongana.

Alisema katika Kata ya Kizwite mitaa iliyofanya uchaguzi ilikuwa 15, ambapo Chadema ilishinda mitaa 13, huku CCM wakiambulia miwili.

Mitaa iliyofanya uchaguzi katika kata ya Msua, ilikuwa 13. Yote imekwenda Chadema. Kata ya Chanji yenye mitaa 14, Chadema imeshinda 10, huku CCM ikiambulia mitatu. Mtaa mmoja uchaguzi utarudiwa.

CCM kilipata ushindi Mtaa wa Bangwe, Kata ya Izia na Chadema ikishinda Mtaa wa Tambazi katika Kata ya Sumbawanga.

Uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu mkubwa tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo ulivurugika katika kata hizo kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza, ikiwa pamoja na vituo kuchelewa kufunguliwa.
Hali hiyo ilisababisha wananchi waliokaa vituoni kwa muda mrefu wa zaidi ya saa nane wakisubiri kupiga kura kuhamaki na kujichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto ofisi ya mtendaji wa Kata ya Kizwite na Kata ya Chanji na kuteketeza nyaraka zote muhimu za kupigia kura.

Hivyo, kufanya mchakato mzima wa uchaguzi huo kurudiwa upya kuanzia kujiandikisha hadi upigaji wa kura.

Chadema ni miongoni mwa vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Vyama vingine vilivyopo katika muungano huo, ni Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League Democrat (NLD).

Ushindi wa Chadema umethibitisha kuwa chama hicho kimeimarika katika ngazi za chini; ukilinganisha na chaguzi zilizopita.

Kwa mfano, katika uchaguzi wa mwaka 2009, CCM kilipata ushindi wa asilimia 91.72, huku wapinzani kwa ujumla wake, waliambulia asilimia 8.28.

Safari ya anguko la CCM imeanza taratibu licha ya makada, viongozi na mashabiki wake kujiapiza kuwa chama chao, hakitang’oka madarakani.

Katika uchaguzi uliopita uliofanyika 14 Desemba 2015, muungano wa upinzani, ungefanya vizuri zaidi kama CCM isingefanya hila. Inararajiwa hila kama hizo zitatokea katika uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba mwaka huu.

CCM kilichozaliwa 5 Februari 1977, kimekuwa na kustawi sana, katika miaka ya 80 na 90. Kilianza kuchuja kuanzia miaka ya 2000 na 2010; na sasa kinaelekea kufa!

Hii itakuwa kwa kusambaratika kabisa, ama kwa kuungana na chama kingine na kuzaliwa chama kipya au hata kwa kung’olewa madarakani.

Katika uchaguzi uliopita – tarehe 14 Desemba 2015 – muungano wa UKAWA ulitarajiwa ungefanya vizuri zaidi iwapo CCM kisingetumia hila kushinda uchaguzi huo. Hila hizo zinatarajiwa pia kutokea uchaguzi mkuu ujao.

Katika uchaguzi huu, CCM ilitumia serikali na vyombo vya dola, kuhakikisha kinaendelea kubaki madarakani.

Makala hii imeandikwa na Mihayo Ally, anapatikana kwa no: 0784-395454

error: Content is protected !!