August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM watakiwa kutobweteka

Spread the love

VIONGOZI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya za Mkoa wa Morogoro, wameshauriwa kuwa wabunifu katika miradi ya maendeleo ya chama hicho, anaandika Christina Haule.

Ni kwa kuwa, ubunifu utasaidia jitihada za Serikali ya Rais John Magufuli katika kukuza uchumi na kwamba, hawatakiwi kubweteka kwa kusubiri misaada kutoka ngazi za juu. 

Mohamed Utaly, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero leo akizungumza kwenye kikao kilichoandaliwa na jumuiya hiyo amesema kuwa, wabunifu na kulipa ada ni jambo litakaloifanya jumuiya hiyo kujiendeleza.

Amesema, wajumbe wengi wamekuwa wakikwepa kulipa ada kwa wakati wakisahau kuwa ada ndio msingi wa chama au jumuiya yoyote na kwamba, bila kulipa ada kwa wakati hawataweza kufanya mambo mengi ya maendeleo wanayokusudia ikiwemo kuanzisha miradi.

Utaly ameishauri jumuiya hiyo kutafuta ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kuwa, wakiwa na ardhi wataweza kukodisha, kuzalisha mazao ama kubinafsha hivyo jumuiya itakuwa na uwezo mkubwa wa kujiendesha yenyewe.

Amebainisha baadhi ya changamoto zinazokwamisha shughuli mbalimbali katika wilaya na jumuiya kuwa ni pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji hivyo kujikuta wakitumia muda mwingi kushughulikia na matatizo hayo.

Amesema, Wilaya ya Mvomero inaukubwa wa eneo la kilometa za mraba 7,325 ambazo ni sawa na hekta 732,500 kati ya hizo hekta 266,400  sawa na hekari 666,000 zinafaa kwa shughuli za ufugaji lakini eneo hilo lina jumuisha mashamba pori ya watu binafsi ambayo hayajaendelezwa, na wafugaji wanayatumia kulishia mifugo yao pamoja na eneo la Ranchi ya Mkata ambapo lina uwezo wa kulisha ng’ombe  133,200.

Amesema, eneo linalohitajika kwa malisho na kwa idadi ya mifugo iliyopo ni hekta 365,850 huku mifugo iliyozidi katika Wilaya ya Mvomero ni 49,725 ambayo inahitaji hekta 99,450 hali inayosababisha  uwiano kutokuwa sahihi kati ya mifugo na eneo la malisho sambamba na kuongeza migogoro katika wilaya hiyo.

Josephat Chacha, Katibu wa jumuiya hiyo Mkoa wa Morogoro amesema, ipo haja kwa viongozi hao kuanzisha sensa ya kuweza kugundua wananchama walio hai.

Ni kwa kuwa, kulikuwepo na baadhi ya wanachama waliokiasi chama hicho kuendelea kuhesabika kama wanachama halali hivyo kushindwa kuwa na muongozo unaoeleweka.

 

error: Content is protected !!