May 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

CCM wataka NDC ing’olewe miradi Mchuchuma, Liganga

Spread the love

 

WABUNGE wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamesema Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), halina uwezo wa kuendeleza mradi wa chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe, Mchuchuma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hivyo, wameishauri serikali kutafuta muwekezaji mpya katika miradi hiyo, kwa kuwa NDC halina uwezo wa kusimamia.

Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa tarehe 9 Aprili 2021 bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo pia Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, wakati wakichangia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo kwa miaka mitano.

Wa kwanza kutoa ushauri huo alikuwa Prof. Muhongo, ambaye alisema NDC haina utaalamu wa kisasa kuendesha miradi hiyo.

Amesema, awali kampuni hiyo ilipanga kuchimba chuma peke yake wakati madini hayo yanabeba madini ya Titanium na Vanadium, ambayo NDC haina ujuzi wa kutosha kuyatenganisha.

“Walikuwa wanataka chuma peke yake, lakini ndani yake kuna Titanium na Vanadium, kwa hiyo mjadala ilikuwa tutapataje, ndiyo maana huu mradi mheshimiwa naibu spika nadhani sijui kama tulifanya vizuri kumpatia mtu mmoja miradi yote miwili.

“Tufanye maamuzi huo mradi upelekwe kwa watu wenye ujuzi wanaojua hayo madini, NDC wamepewa mradi kule Ngaruka, hawawezi na wao watolewe, NDC kama imeshindwa kuendeleza mradi kwa miaka zaidi 40, sidhani kama wana uwezo huo, na kweli hawana.”

Mbunge Shangazi ameungana na Prof. Muhongo akisema, kampuni hiyo haina uwezo wa kuchimba madini hayo.

“Tumepata somo zuri kutoka kwa Prof. Muhongo, lakini amezidi kutufundisha kwamba, kuna maeneo sisi kama Taifa ni lazima tuongeze umakini na tufanyie kazi kwa uharaka ili tufanane na wenzetu,” amesema Shangazi na kuongeza:

“…na nikianzia alipoishia, uwezo wa NDC kuendesha mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma, ni kweli wasiwasi huo sio tu yeye anao, lakini wabunge wengi wanaotoka maeneo hayo, wanajiridhisha hivyo.”

error: Content is protected !!