January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM washtakiana kwa Kinana

Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Sumar Shaffin Ahmedali

Spread the love

JOTO la uchaguzi mkuu linazidi kupanda ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na sasa makada wake wameanza kushitakiana wakituhumiana kuanza kampeni kabla ya wakati. Anaandika Edson Kamukara…(endelea).

Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Sumar Shaffin Ahmedali, amewasilisha malalamiko kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akidai kuchafuliwa katika jimbo lake.

Sumari anamtuhumu Almasi Athumani Maige-ambaye alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba- kuanza kampeni kabla ya wakati na kinyume cha taratibu.

Almasi anaaminika kuwa mtu wa karibu sana na Shabani Gurumo na Bernard Membe ambaye anatajwa kuwa mgombea urais kupitia CCM.

Katika barua yake ya kurasa tatu ya Februari 12 mwaka huu, kwa Kinana, Sumari anasema, “…ni jambo linalonishangaza kuona huyu anayejiita kada wa CCM baada ya kuibuka mwaka 2015, kuendelea kutoa misaada ya hali na mali katika jimbo hili.”

Anasema, Maige anajitokeza kutembea na kutoa misaada katika jimbo hilo pekee, wakati wilaya ya Uyui, ina majimbo mawili ya uchaguzi.

“Nachukua nafasi hii kufikisha malalamiko yangu kuhusu Katibu wa UVCCM Wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora, Mohamed Salmin kukiuka kanuni za uchaguzi za CCM kwa kujihusisha na vitendo vya kampeni katika jimbo la Tabora Kaskazini,”amesema.

Kwa mujibu wa malalamiko hayo, Sumari anasema katibu huyo amekuwa akimtembeza na kumnadi Maige ambaye anajiita kada wa CCM.

Anasema kuwa katibu huyo, amemtembeza Maige katika kata kadhaa za jimbo hilo na kumkutanisha na vijana pamoja na wanachama wengine wa CCM ambapo ametumia fursa hiyo kujitambulisha na kueleza nia yake ya kugombea ubunge mwaka huu.

“Januari 5 mwaka huu, katibu wa UVCCM wilaya ya Uyui akishirikiana na Mwenyekiti wake, Shaban Katalambula, waliitisha kikao cha kamati ya utekelezaji na kumteua Maige kushika wadhifa wa naibu kamanda na mlezi wa UVCCM wilaya,” anaandika Sumari katika barua yake.

Sumari anakwenda mbele zaidi akidai kuwa; Januari 7 mwaka huu, saa 4:30 asubuhi, wakitumia gari aina ya Nissan Patrol V8 yenye namba za usajili T811 DCR pamoja na magari mengine, katibu huyo wa UVCCM alimpeleka Maige katika kata ya Ufulama ambapo alionana na kuzungumza na wananchi wa vijiji vya Ufulama na Chesa.

Pia, Maige anadaiwa kutoa mchango wa shilingi 500,000 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya CCM kata ya Ufuluma na shilingi 300,000 kama malipo ya mshahara wa mlinzi wa mti ulioanguka na kusimama kimiujiza katika kijiji cha Chesa.

Sumari anaendelea kulalamika kuwa; pia Januari 7 mwaka huu, katibu huyo alimpeleka Maige katika kata ya Ndono ambapo alikutana na viongozi wa CCM kata na tawi na kutangaza nia ya ubunge huku akichangia shilingi 450,000 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya chama.

Vile vile Januari 8, Maige anadaiwa kupelekwa kata ya Bukumbi na kukutana na wajumbe wa NEC ambao aliwalipa posho ya shilingi 5,000 kila mmoja na kufanya hivyo tena katika kata ya Isikizya Januari 9.

Maige na Salmin hawakupatikana kufafanua tuhuma dhidi yao na vile vile Kinana kwa siku nzima hakupokea simu ili kudhibitisha kama amepokea barua hiyo. Hii ni kutokana na kuwa katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM).

error: Content is protected !!