July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM wapingana kuhusu utawala wa Magufuli

Spread the love

UTAWALA wa Rais John Magufuli umeibua mjadala kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Rorya, Mara na hata kusababisha kuibuka makundi mawili, anaandika Moses Mseti.

Kundi moja linaonesha kuwa na imani na Rais Magufuli kwa hatua anazochukua katika utawala wake huku lingine likiutaja utawala wa kiongozi huo kuwa wa mabavu.

Kinachoendelea ndani ya CCM kwenye wilaya hiyo ni kuwepo kwa madai ya kuhujumiana kwa siri kwa kile kilichoelezwa kuwa, kundi moja linapinga utawala wa Rais Magufuli kwa kuwa hawaridhiki nao.

Makundi yaliyoibuka ya madiwani wa chama hicho ambapo miongoni mwao wanaonesha kudharau na kukebehi baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli.

Miongoni mwa m madiwani wanaotajwa kuwemo kwenye sakata hili ni pamoja na Mariam Odunga na Anna Dhaje.

Mtandao huu ulimtafuta Samweli Keboye, Mwenyekiti wa Wilaya ya Rorya ambaye alikiri kuwepo kwa hali ya sintofahamu kwa baadhi ya viongozi wa kuteuliwa na kuchaguliwa (madiwani) ndani ya wilaya hiyo.

“Ni kweli kuna barua ilifikishwa mezani kwangu kutoka kwa wanawake wa hapa wilayani ambao ni wanachama wa CCM wakinitaarifu kwamba, hawafurahishwi na mwenendo wa baadhi ya madiwani katika kuheshimu viongozi, sasa wakataka kufanya maandamano ya amani tarehe 24 mwezi huu ili kuwafikishia ujumbe.

“Baada ya kusoma barua yao nimeamua kuyazuia maandamano hayo kwani wanaweza kutumia njia nyingine ya kuwafikishia ujumbe hata kwa kuitisha vikao vya chama,”amesema.

Keboye amesema, wapo baadhi ya madiwani wamekuwa wakitoa lugha zisizofaa na zilizo na mwekeleo wa kumchafua yeye binafsi, Lameck Airo, Mbunge wa Jimbo la Rorya, na Charles Ochele, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

“Kuna watu ndani ya chama chetu wanajifanya ni watiifu lakini ni wanafiki wakubwa, unapowauliza wanakana na kujifanya ni watiifu kumbe ndio wanaoharibu chama chetu.

Kwa upande wa Odunga , alisema yeye ni mtiifu kwa viongozi wake na anashirikiana na kila mmoja.

“Suala la kuwepo maandamani mimi sijui lakini ninachoweza kusema huwa sina tabia ya kudharau au kumhujumu mtu, sina ugomvi na mwenyekiti wangu wala mbunge, wote hao nimekuwa sambamba nao kuanzia kipindi cha kampeni za mwaka jana hadi sasa.

“Mimi nilikuwa miongoni mwa mawakala mwa mbunge na tulishirikiana na Keboye hadi mwisho, nipo tayari kumtafutia mwenyekiti kura atakapogombea, tena sasa iweje tukosane,”amehoji.

Diwani Dhaje amesema, tangu ajiunge na CCM mwaka 1978 na kuwa diwani wa viti maalum kwa wakati tofauti hajawahi kudharau viongozi wake.

Dhaje amekana kuhusika kwa namna yoyote ya kuwahujumu au kutoa lugha chafu kwa viongozi hao na kusisitiza kwamba, ataendelea kushirikiana na kila mtu.

error: Content is protected !!