August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM wanakumbatia staili ya ‘Chura’

Spread the love
HIVI sasa, kutokana na staili yake na ya kundi analoongoza la Wasafi. Mwimbaji na msanii wa miondoko ya kizazi kipya, Naseeb Abdul – ‘Diamond’, amejizoelea umaarufu mkubwa, huku vijana na hata baadhi ya ‘wazee vijana’ wakitaka kufanana naye, anaandika Adam Mwambapa.
Hii ni kutokana na umaarufu wake. Na hivyo basi, kila anachokifanya, hata kama ni cha kawaida sana, nacho hugeuka maarufu.
Umaarufu ni jambo ambalo kila mmoja hulitaka. Licha ya kuwa, hakuna umaarufu usiokuwa na gharama ama athari zake, lakini pamoja na yote – unatakiwa.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), nacho kimekuwa kikiutafuta usafi na umaarufu kwa gharama yoyote ile. Na kimekuwa kikijifananisha waziwazi na mwanamuziki Diamond.
Licha ya kwamba, CCM imekuwa ikicheza staili ya ‘chura’ ikiwa ni tofauti kabisa na ile inayotumiwa na Wasafi.
Chura, ni staili inayotumiwa na msanii wa kizazi kipya na mwigizaji wa michezo ya kuigiza, Snura, ambayo, licha ya vionjo vyake kuwa vya hovyo, inaendelea  kujizolea umaarufu.
Staili ya mchezo huo ‘chura’ inayochezwa na Snura, imeonesha kuwa haifai hata mbele za jamii iliyostaarabika. Wimbo wake, pamoja na staili hiyo ya ‘chura’ inaelezwa imefungiwa na serikali.
Hivi sasa wimbo huo, hauruhusiwi kupigwa au kuonekana kwenye kituo chochote cha radio au televisheni nchini.
Mchezo au staili ya ‘chura’, naulinganisha kabisa na michezo mingi inayofanywa kila mara na baadhi ya viongozi na wafuasi wa CCM.
Viongozi wanaofisidi, wanaodhulumu, wanaotapeli na kuhamisha mali na raslimali za nchi, wengine wakiwa ni watuhumiwa wa wizi na utoroshaji wa fedha kwenda ughaibuni, lakini kwa CCM ni waadilifu na baadhi wakiwa viongozi wa Bunge.
Viongozi wa CCM wamekuwa wakipiga ngoma nyingine na kucheza mirindimo ya ngoma nyingine. Huku wakihadaa wananchi kama wanacheza ngoma ileile wanayoipiga.
Watajitofautishaje na staili za ‘chura’ wakati bado ndani yao, kuna viongozi wanaowalipa wafanyakazi hewa, wanatengeneza mishahara hewa kiasi cha mtu mmoja kuwa na mishahara 17?
Au mwanachama wa CCM kumiliki nyumba zaidi ya 70 katika nchi ambayo inapinga ubepari na unyonyaji, yenye kufuata misingi ya usawa na umoja kwa raia wake?
Taarifa za mfanyakazi mwenye beji ya CCM, ambaye amekuwa akipokea mishahara hiyo zaidi ya 17 na kuiibia serikali ya chama chake kwa miaka nenda miaka rudi je, huyu anacheza staili gani na viongozi wake kama siyo ile ya chura?
Ieleweke kuwa serikali ya CCM iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, ndiyo iliyochangia na kuonekana kuipa kazi ngumu awamu hii – ikiongozwa na Dk. John Magufuli.
Ndiyo maana sasa Rais Magufuli amejipa kazi ngumu ya kutumbua  majipu, hata  kama anafanya usanii, lakini ameachiwa kazi ngumu sana, tena inayoonekana itakwama mapema.
Ni jambo la ajabu zaidi, kwamba CCM wanaendelea kuwaaminisha wananchi kwamba maisha ya wananchi yamekuwa bora zaidi wakati siyo kweli. Maisha ya wengi ni mabaya mno, licha ya kuelezwa  kuwa uchumi na pato  la taifa limepanda. Eti uchumi wetu unakua kwa asilimia 7, ajabu!
Hiyo haina tofauti na kile kilichoamishwa kwa wafanyakazi – Siku Mei Mosi ya mwaka huu na Rais John Magufuli.
Rais alisema kuwa kodi katika mishahara ya wafanyakazi (PAYE)- imepunguzwa kutoka asilimia 11 – hadi 9, wafanyakazi walishangilia kwa nguvu mara baada ya kisikia hivyo, lakini ukweli ni kwamba uamuzi huo hautawasaidia watumishi.
Kwa hesabu za haraka, kiasi hicho ni Sh. 1,100 ndiyo kitapunguzwa kwa wale wanaopokea kuanzia Sh. 175,000 hadi 360,000 na Sh. 3,200 zitakatwa kwa wale wanaopokea kuanzia Sh. 361,000 hadi milioni moja, kwa edha liyotangazwa imepunguzwa kodi, hivi kwa kiasi hicho kitaleta nafuu gani kwa mfanyakazi? Kiasi hiki ni kidogo sana na hakipaswi kushangiliwa.
Ni kweli wasomi wetu wafanyakazi, wamekosa uelewa wa kukichambua na kukitofautisha kiasi cha ongezeko au punguzo la asilimia 2? Kama ndivyo, basi tumeshikwa pabaya.
Niliwahi kusema huko nyuma kwenye makala zangu.Nikasema, miongoni mwa mambo ambayo Dk. Magufuli yanampa shida ni eneo la mishahara.
Kwa uamuzi huo, hakika CCM hawana nia ya dhati kumkwamua Mtanzania na mfanyakazi kwa ujumla.
CCM wameendelea kuwaongopea wananchi- Hawatosheki kwa uongo, wao ni kuwarubuni tu wananchi. Waliahidi  – maisha bora kwa kila Mtanzania, chini ya kaulimbiu ya ‘Ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya’ yaani (Anguka), ikawashinda.
Japokuwa hiyo Anguka ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya waliokuwa kwenye mtandao tu! Ndiyo ari mpya ya kuiba, nguvu mpya ya kupiga madili na kasi mpya ya kulifilisi taifa, ilikuwa ndani ya uwezo wao.
Ni katika kipindi hicho kukatokea wizi wa mabilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Mfuko wa Madeni ya Nje (EPA), baadaye ikawepo “zimwi” la Kagoda Agriculture, Meremeta, Dowans, Symbion na karibuni wakaja na Tegeta Escrow.
Hakika CCM wanacheza staili ya chura na kujisifia kwamba wao ni Wasafi – wafuasi wa Diamond.
 
·  Simu: 0765/0713 937 378 au Barua Pepe:amwambapa7@gmail.com
error: Content is protected !!