Spread the love

 

WAKATI chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikielekea kufanya mkutano mkuu maalum tarehe 1 Aprili 2022, baadhi ya wanachama wa chama hicho wameanza kumtaka Dk. Ali Mohamed Shein kumwachia Rais Hussein Ali Mwinyi nafasi ya umakamu mwenyekiti wa chama hicho, visiwani Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Shein alimaliza muda wake wa uongozi wa urais wa Zanzibar tarehe 2 Novemba 2020 wa miaka kumi na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Mwinyi aliyeibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekuwa taratibu kwa viongozi wanapomaliza muda wao wa uongozi hususan nafasi ya urais, huwaachia uongozi kwenye chama kwa maana ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti-Zanzibar.

Hii imekuwa ikishuhudiwa ikitokea mara kadhaa na sasa wadadisi wa masuala ya siasa hususan visiwani Zanzibar waliozungumza na gazeti hili, wanaona umefika wakati wa Dk. Shein kumwachia nafasi hiyo Rais Mwinyi ili aweze kuongoza chama na Serikali kwa pamoja.

Wanaeleza hayo ikiwa zimesalia takribani siku kumi kufanyika kwa mkutano mkuu huo maalum ambao pamoja na mambo mengine utafanya marekebisho ya katiba ya chama hicho ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Hata hivyo, Chama Cha Mapindizi (CCM) visiwani humo kimesema, Dk. Shein hajasema sehemu yoyote kwamba anakwenda kung’atuka na kumwachia nafasi hiyo Rais Mwinyi kwani hilo ni la kwake yeye (Shein) kujipima na kutafakari nini anapaswa kukifanya.

Kimesema, nafasi hiyo ni ya kuchaguliwa hivyo hapaswi kulazimishwa kuachia licha ya utaratibu wa kuachiana upo na binafsi kinaungana na wale wanaosema umefika wakati wa Dk. Shein kukaa kando ili Rais Mwinyi awe na fursa ya kuongoza chama na serikali.

Mmoja wa makada wa CCM visiwani Zanzibar aliyezungumza na gazeti hili alisema, “mkutano huu sasa ni wakati wa Dk. Shein kumwachia Rais Mwinyi umakamu mwenyekiti, ili anapoinyoosha nchi serikalini awe na uwezo wa kufanya hivyo na kwenye chama, kwa sasa hawezi.”

“Tulitarajia kwenye ule mkutano mkuu uliomchagua Rais Samia (Suluhu Hassan) kuwa mwenyekiti, naye angemwachia Mwinyi lakini haikuwa hivyo, sasa huu ni wakati sahihi na ikizingatiwa ni wakati wa uchaguzi,” aliongeza.

Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM

Mkutano anaozungumzia ni ule uliofanyika tarehe 30 Aprili 2021 jijini Dodoma ambao ulimchagua kwa asilimia 100, Rais Samia kuwa mwenyekiti wa chama hicho, akichukua nafasi iliyokuwa imeachwa na Hayati Rais John Pombe Magufuli.

Hayati Magufuli, alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam na mwili wake kuzikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita.

Mtandao huu ulimtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Catherine Nao kuhusu suala hilo ambapo alisema Dk. Shein hajasema popote na hakuna kikoa chochote cha chama alichosema kama atang’atuka “na hatuwezi kumsemea hilo ni la kwake.”

Akizungumzia minong’ono ya baadhi ya wana CCM kutaka Dk. Shein amwachie Rais Mwinyi uongozi wa chama, Catherine alisema, “wanaweza kuwa na mawazo lakini nafasi hii niyakuchaguliwa, anapaswa mtu awe na ridhaa yake mwenyewe ya kuondoka na hatujajua kama hiyo anayo.”

“Yawezekana anasubiri mkutano mkuu akaseme pale pale lakini hii nafasi ni ya kuchaguliwa na ingekuwa ya kuteuliwa unaondoka baada ya kuteuliwa mwingine, kwa hiyo ana ridhaa yake, kuondoka ama kutoondoka na hakuna wa kumlazimisha,” alisema

Kuhusu hoja ya Rais Mwinyi kushindwa kukinyoosha chama kama ambavyo anafanya serikalini kwa watumishi kuteua na kutengua ili kuweka ufanisi, Catherine alisema, “wanachokisema watu wanaona hivyo, lakini kama nilivyosema, hii ni nafasi ya kuchaguliwa, hawezi kulazimishwa kumwachia.”

Akijibu swali aliloulizwa, iwapo jitihada za wazee wa chama kumshauri Dk. Shein amwachie nafasi hiyo Rais Mwinyi, katibu huyo wa itikadi na uenezi alisema “kwa jambo hili hakuna kushauri, ni yeye mwenyewe tu kutafakari na kujiongeza, kuwa sasa nimwachie.”

CCM kinakwenda kufanya mkutano huo maalum jijini Dodoma kurekebisha na kupitisha katiba kwani mamlaka hayo yako mikononi mwa mkutano mkuu wa Taifa wa CCM, chini ya ibara ya 99 (5), toleo la 1977.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka akizungumza na waandishi wa habari 12 Machi mwaka huu kutoa maazimio ya kakamti kuu iliyofanyika siku moja kabla alibainisha mambo yanayokwenda kufanyika.

Shaka alitaja malengo matano ya marekebisho hayo, kwamba ni mosi, kuongeza ufanisi wa kazi za chama na utekelezaji wa uamuzi wa vikao vyake.

Pili, ni kupata viongozi imara, waadilifu na wenye uwezo mkubwa wa kuongoza na kusimamia majukumu ya serikali za mitaa, kwa ufanisi.

Tatu, ni kuongeza na kuimarisha udhibiti wa chama kwa viongozi wanaochaguliwa kuongoza na kusimamia utekelezaji Ilani ya CCM, kupitia serikali za mitaa na kuimarisha nguvu ya chama kukabiliana na kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka na rushwa.

Nne, ni kuongeza uwakilishi wa jumuiya za CCM ngazi ya kata, kwenye mkutano mkuu wa wilaya na kurekebisha itifaki za uwakilishi unaofanana na wenyeviti na makatibu wa jumuiya mkoa, kuwa wajumbe wa mkutano mkuu na wa ngazi ya wilaya kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa.

Mbali na malengo hayo, Shaka alisema CCM inafanya mabadiliko ya Katiba katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wake wa ndani, kwa ili kujiimarisha.

“Kwa nyakati hizi ambazo tunaelekea kwenye uchaguzi, niseme CCM tumekuwa na utaratibu wa kujiimarisha nyakati zote tangu 1977, baada ya kuundwa kwake. Kwa vipindi tofauti imekuwa na utaratibu wa kujiimarisha,” alisema Shaka.

Aliongeza kuwa kuna maeneo ambayo kama chama, wanahisi hawajafanya vizuri, kwa hiyo maeneo hayo wanakwenda kujiimarisha.

Alisema, marekebisho hayo yatawarejesha makatibu wa CCM wa mikoa kwenye ujumbe wa NEC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *