August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM wamnunia JPM

Spread the love

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameingia kihoro kwa Rais John Magufuli baada ya kubanwa, anaandika Pendo Omary.

Hatua hiyo inatokana na kutorekebishwa chochote kwenye bajeti yake hasa makato ya fedha za kiinua mgongo kwa wabunge hao ambao dhahiri walionekana kutofurahishwa.

Hata hivyo, Dk. Philip Mpango amewaambia kwamba, wao pamoja na Watanzania wengine ndio waliomchagua Rais Magufuli hivyo ‘wafunge mkanda’ ili atimize malengo yake.

Lakini pia mguno wa wabunge wa CCM ni kutokana na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/17 kupita kama ilivyowasilishwa na Dk. Mpango huku marekebisho machache yasiyowahusu yakifanyika.

Licha ya wabunge wa CCM kupinga kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao na kuwa na matumaini ya marekebisho eneo hilo, serikali iliwasilisha mpango wa kuongezwa wakatwaji kodi akiwemo Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu pia wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

Hatua ya kuongezaa viongozi hao wa juu ilizima matumaini ya wabunge hao kuondolewa kodi hiyo ambayo ilionekana kuumiza mioyo yao wazi wazi.

Hata hivyo jana Dk. Mpango aliwaambia waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi katika baadhi ya maeneo ya bajeti hiyo kwamba, utawala wa Rais Magufuli ni kwa kila mtu kulipa kodi.

Amefafanua kuwa, maendeleo ya taifa pia ya mtu mmoja mmoja si jambo la lele mama na kwamba, kila mmoja anapaswa kulipa kodi ili taifa lifikie malengo yake ya kuwa na uchumi bora.

“Maendeleo hayaji kwa njia ya ujanja, kila mmoja anapaswa kulipa kodi. Watanzania lazima walipe kodi,” amesema.

Kwa upande wa kodi katika taasisi za dini Dk. Mpango amesema, utaratibu uliopo ni tofauti na ule wa awali.

Amesema, baada ya kujiridhisha kwamba taasisi za dini hazina fedha, sasa taasisi hizo zinapoagiza vitu kutoka nje zinapaswa mwanzoni mwa mwaka kuwasilisha orodha ya vifaa na vitu itakavyoagiza kutoka nje sambamba na kutaja vitu na vifaa vilivyopata msamaha katika mwaka uliopita.

Pia kuwasilisha majina ya watu watakaokuwa na dhamana na watakaosimamia utoaji wa vifaa hivyo bandarini, kutaja jina na wakala wao pia barua ya mkuu wa wilaya na mtendaji wa kata.

error: Content is protected !!