August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘CCM wamempuuza Waziri Mkuu’

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepuuza kauli ya Kassimu Majaliwa, Waziri Mkuu iliyowataka wananchi kuacha na siasa na kujikita katika maendeleo, anaandikaFaki Sosi.

Waziri Majaliwa alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa mwaka huu alipokwenda jimboni kwake Ruangwa kwa ajili ya mapumziko.

Kain Mwakanyemba (Chadema), Diwani wa Kata ya Nkuyu katika Halmashauri ya Kyela, Mbeya amesema, viongozi wa wamepuuza wito huo kwa sababu za kisiasa.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwenye ofisi zao jijini Dar es Salaam leo Mwakanyemba amedai, viongozi wa CCM wamekuwa mstari wa mbele kupinga maendeleo ya wananchi kutokana na utashi wao wa kisiasa.

Amesema kuwa, viongozi hao wanapanga mikakati ya kutowapa ushirikiano madiwani wa upinzani ili kata zao zidode na hatimaye kuonekana hawajafanya kazi.

Amedai moja ya mikakati ya CCM ni pamoja na kujimilikisha Mnara wa Simu unaolipiwa kodi katika eneo la Bosikali lilipo kwenye kata yake na kwamba alipanga kutumia fedha hiyo ya kodi kwa maendeleo ya kata.

Amesema, mnara huo unaomilikiwa na Kampuni ya Simu ya Mikononi wa Airtel ulikuwa unachangia fedha ambazo zingeweza kusaidia kuboresha huduma za jamii.

Amesema, licha mnara huo kubinafsishwa na viongozi wa CCM ambao walikuwa madarakani kabla yake, alikuwa na mpango wa kuurudisha mikononi mwa wananchi.

Amesema kuwa, mikakati mengine inayofanywa na viongozi wa CCM ni kuzuia kuundwa kwa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Kyela ambao kwa sasa ni Mamalaka ya Mji Mdogo wa Kyela wenye sifa za kuwa Halmshauri ya Mji mdogo.

Diwani huo amesema kuwa, matokeao ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana ndio chanzo cha kupingwa kuundwa kwa Halmashauri ya Mji mdogo kutokana na mamlaka hiyo ya Mji Mdogo kuwa na madiwani 14. Madiwani wanane wa Chadema na sita ni wa CCM.

Mwakanyemba amesema kuwa, idadi ya madiwani wa Chadema katika baraza hilo la Mamlaka ya Mji huo imesababisa kupanga mikakati hiyo.

“Jambo hilo kwa upande wangu mimi naona hawa watu wa CCM wana uruho wa madaraka lakini pia ni wabakaji wa demokrasia,” amesema.

Pamoja changamoto hiyo Mwakanyemba amesema kuwa, safari yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata ya Nkuyu tayari imeanza.

Amesema kuwa mkononi mwake anadeni la elimu, afya, maji na miundombinu kwa wakazi wa kata hiyo.

error: Content is protected !!