August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM wakwaa kisiki Morogoro

Suzan Kiwanga

Spread the love

MAHAKAMA kuu ya Tanzania imetupilia mbali mashtaka mawili ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyofunguliwa dhidi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika majimbo ya Kilombero na Mlimba mkoani Morogoro, anaandika Christina Haule.

Kesi ya kupinga ushindi wa ubunge katika jimbo la Mlimba ilifunguliwa na Godwin Kunambi huku ile ya jimbo Kilombero ikifunguliwa na Aboubakar Asenga ambapo wote wawili ndiyo waliokuwa wagombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika majimbo hayo.

Akisoma hukumu ya kesi dhidi ya Peter Lijualikali mbunge wa CHADEMA jimbo la Kilombero, Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania Projest Rugazia amesema,  kesi hiyo Na. 6 ya mwaka 2015 ilikuwa na mpambano mkali kati ya mawakili wa pande zote mbili.

Jaji huyo amesema hoja zilizopelekwa mahakamani hapo ikiwemo za kutumika kwa lugha za kashfa, maudhi, matusi na ubaguzi wa kikabila, mashahidi 7 waliotoa ushahidi akiwemo mgombea wa CCM mwenyewe walishindwa kuthibitisha madai yao pasipo kutiliwa shaka.

Jaji Rugazia alidai pindi walipoulizwa maswali na mahakama na mashahidi hao walionekana kurudia rudia jambo ambalo limeidhihirishia mahakama kuwa huenda mashahidi walifundishwa maneno waliyosema, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Jaji huyo alisema, kufuatia hilo mahakama haioni mashaka kwa mbunge wa sasa Lijualikali kuendelea na nafasi yake ya kuwatumikia wananchi huku akimtaka mlalamikaji Asenga kulipia gharama za kesi hiyo na rufaa ikiwa wazi atataka kupinga uamuzi huo.

Baada ya hukumu hiyo, mbunge Lijualikali aameeleza kushangazwa na nguvu kubwa iliyotumiwa na Jeshi la polisi ili kuwatisha wananchi waliokuwa wakielekea mahakamani kusikiliza hukumu ya kesi hiyo.

Mbunge huyo amewashukuru wananchi, chama na viongozi wake kwa kushirikiana naye mwanzo hadi mwisho wa kesi hiyo na kuahidi kununua gari la kubebea wagonjwa kwa kutumia fedha zitakazopatikana baada ya malipo ya uendeshaji wa kesi hiyo.

Katika Kesi ya Pili dhidi ya Mbunge wa jimbo la Mlimba Suzane Kiwanga, Jaji Panterine Kente ametoa uamuzi wa ametupilia mbali shauri lililofunguliwa na Godwin Kunambi baada ya kutoridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mlalamikaji.

Jaji huyo alisema kuwa katika shauri hilo mlalamikaji alipinga matokeo ya ushindi wa mbunge huyo kwa madai ya kutoridhishwa na mchakato mzima wa zoezi la kampeni na lile la upigaji kura sambamba na matokeo ya uchaguzi akihusisha na masuala ya rushwa.

Godwin Kunambi aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Mlimba CCM mara baada ya hukumu hiyo amesema haridhishwi na maamuzi yaliyofikiwa na Mahakama hiyo, hivyo atakata rufaa.

Mbunge wa Mlimba Suzan Kiwanga, naye atakaa na viongozi wake kuhakikisha wanafungua kesi ya madai juu ya kesi hiyo kufuatia kupoteza muda mwingi kwenye kesi badala ya kuwatumikia wananchi waliomchagua.

Kesi hizo ziliendeshwa katika kipindi cha miezi 9 katika mahakama ya wilaya Kilombero na hatimaye leo zimetolewa hukumu na mahakama mbele ya majaji tofauti.

Hajra Mwungula ndiye aliyekuwa wakili wa upande wa mlalamikaji katika Jimbo la Kilombero ambapo alikabiliana na wakili Peter Kibatara wa Chadema huku katika jimbo la Mlimba wakili Yassin Memba (CCM) akikabiliana na Tundu Lissu wa Chadema.

Majimbo ya Kilombero na Mlimba ni majimbo jirani yakiwa katika wilaya moja ya Kilombero ambapo jeshi la polisi liliimarisha ulinzi na doria kuanzia Julai 27 na hata kuongeza nguvu ya askari kutoka mikoani na hivyo kuzua hofu kubwa kwa wananchi.

 

error: Content is protected !!