Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa CCM ‘wakaidi’ agizo la Jaji Mutungi
Habari za SiasaTangulizi

CCM ‘wakaidi’ agizo la Jaji Mutungi

Katibu Mkuu CCM Daniel Chongolo katika moja ya ziara zake
Spread the love

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), “kimeendelea kukaidi,” maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi, aliyeomba kusitishwa kwa mikutano ya ndani ya vyama vya siasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Septemba 2021, Jaji Mutungi “alielekeza” vyama vya siasa, kusitisha shughuli zao, hadi hapo kutakapofanyika mkutano kati ya mkuu wa jeshi la polisi (IGP) na wadau wa siasa nchini.

Jaji Mutungi alisema, lengo la kikao hicho ni kuondosha mvutano uliojitokeza kati ya polisi na vyama vya siasa, na kwamba mazungumzo hayo yanalenga kumaliza mvutano huo.

Mkutano kati ya vyama vya siasa na viongozi wakuu wa polisi, umepangwa kufanyika jijini Dodoma, tarehe 21 Oktoba 2021.

Alisema, “tunakwenda kuelimishana namna bora ya kufanya kazi zetu za kisiasa vizuri zaidi.” Akawaomba wadau wa siasa, kumpa nafasi ili aweze kuandaa kikao hicho kitakachomhusisha Simon Sirro, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

Wakati Jaji Mutungi akitaka vyama kusubiri kikao hicho, uongozi wa CCM umeamua kufanya ziara katika mikoa kadhaa nchini, ikiwamo Lindi, Mtwara, Ruvuma na Njombe.

Ziara ya viongozi hao, ambayo ililenga kuimarisha chama na kukagua miradi ya maendeleo, ilianza tarehe 15 Septemba na ilikamilika juzi Jumanne, 21 Septemba.

Miongoni mwa viongozi wandamizi walioshiriki ziara hiyo, ni Daniel Chongolo, katibu mkuu wa chama hicho. Chongolo aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC).

Miongoni mwa wajumbe hao; ni Naibu Katibu Mkuu-Bara, Christina Mdeme, Katibu wa Itikadi na Unenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka pamoja na Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.

Naye Job Ndugai, Spika wa Bunge na Mjumbe wa kamati kuu ya CCM, alifanya ziara kama hiyo, Visiwani Zanzibar.

Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga

Ndugai ambaye ametambulishwa na chama chake, kuwa mlezi wa CCM katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja, alifanya ziara hiyo, kati ya tarehe 20 na 21 Septemba.

Alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume na Bandari, kwa kile kilichoitwa, “ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM yam waka 2020 hadi 25.”

Hata hivyo, maeneo ambayo Ndugai alitembelea, hayako katika mikoa ambayo inaelezwa na chama hicho kuwa yeye ni mlezi wake. Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar, uliyopo Unguja, upo mkoa wa Mjini Magharibi, sambamba na bandari ya Malindi.

Kassim Majaliwa Majaliwa, waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano, alikuwa kwenye ziara ya kiserikali mkoani Kigoma.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Christina Mndeme akiwa katika moja ya ziara yake

Ikiwa Kigoma alijivisha kofia ya ujumbe wa Kamati Kuu na kufanya kikao chama chake – halmashauri kuu ya mkoa (NEC) – kinyume na misingi ya utawala bora na maelekezo ya Jaji Mutungi.

Majaliwa alikuwa Kigoma, kati ya tarehe 16 Septemba 2021.

Katika mkutano huo, Majaliwa alimpokea kada wa ACT-Wazalendo, Adibily Kazala na kumkabidhi kadi ya CCM. Kazala alikuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Kasulu Vijijini.

MwanaHALISI Online, limeshindwa kuwapata viongozi wajuu wa chama hicho, kueleza kinachowasukuma kukaidi maelekezo ya msajili.

Yumkini wakati CCM wakifanya ziara hizo na kukutana na wanachama wao, vyama vya upinzani vimekutana na zuio la polisi.

Moja ya chama ambacho kimezuiwa kufanya shughuli zake, tena za kikatiba, ni NCCR – Mageuzi, kilichozuiwa kufanya mkutano wake wa Kamati Kuu.

Kikao hicho chenye wajumbe wasiozidi 30, kilikuwa kifanyike tarehe 28 Agosti 2021, katika ukumbi wa Msimbazi Center jijini Dar es Salaam.

Maofisa wa polisi walidai kuwa mkutano huo, umezuiwa kufanyika kwa sababu ya kuwapo kwa maambukizi ya corona na kile walichokiita, “maelekezo kutoka juu.”

Kilichokutana nacho NCCR-Mageuzi, ndicho kimekuwa kikiwasibu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa takribani mwaka mmoja sasa.

Polisi kwa sababu wanazozijua wao, kimezuia makongamano ya kudai katiba mpya na mikutano ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Wanawake wa Chadema, walijikuta wakipata zuio la kufanya mazoezi ya asubuhi ‘jogging,’ tarehe 18 Septemba 2021, kwa madai kuwa mazoezi hayo hayawezi kufanyika wakiwa wamevaa tisheti za kudai katiba mpya.

Bawacha walilaani kitendo hicho, huku Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai akiwaonya kuwachukulia hatua.

Akizungumzia maandalizi ya kikao hicho hivi karibuni, Jaji Mutungi alisema yanakwenda vizuri na unatarajiwa kuongozwa na mtu ambaye hana mgongano wa maslahi.

“Kikao cha wadau kikiendeshwa na IGP kinaweza leta taswira IGP huyo huyo ndiyo tunamlalamikia, kikiendeshwa na msajili, msajili huyo huyo tuna madudu yake tunataka kuyasema, mwenyekiti wa uendeshaji kikao atakuwa mtu neutral,” alisema Jaji Francis.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Vijana ACT-Wazalendo Dar wampa tano Rais Samia

Spread the love  NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, kimempongeza Rais...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yaiangukia Serikali kunusuru wananchi Liwale, Nachingwea

Spread the love  CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka...

Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wanaokwamisha mradi Liganga na Mchuchuma kitanzani

Spread the love  NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, watu wanaokwamisha utekelezaji...

Habari za Siasa

Gridi ya Taifa kufumuliwa kukabiliana na katizo la mgao wa umeme

Spread the love  WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba, amesema Serikali ina mpango...

error: Content is protected !!