July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM waache ‘shingo feni’

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa akiwa na viongozi wa Chadema, kushoto ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu

Spread the love

WAKATI najiandaa kuandika makala hii, waziri mkuu wa kwanza katika awamu ya nne, Edward Ngoyai Lowasa, ametangaza kukihama chama chake cha CCM na kujiunga na Chadema kilichoko katika muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Uamuzi huu umehitimisha tetesi nyingi zilizozagaa mitandaoni zikiibua mambo mengi kuhusiana na mwanasiasa huyu mkongwe na mwenye ushawishi mwingi.

Kabla ya Lowassa kutamka kujiunga na Chadema, yamekuwapo maneno mengi kutoka chama tawala na jitihada nyingi za kutaka kumzuia asiondoke chama hicho.

Iliposhindikana kumzuia, yalifuata maneno ya kuwakatisha tamaa Chadema ili wasimpokee. Hilo nalo liliposhindikana, yalifurika matusi na vitisho vingi kwa Lowassa kuwa atashitakiwa yeye na marafiki zake. Kwa hiyo, tangazo la Lowassa ni hitimisho la msururu wa vitimbi vya kisiasa kutoka CCM kwenda Chadema na kwa Lowassa mwenyewe.

Tangu mwaka 2008, wakati Lowassa alipojiuzuru nafasi yake ya uwaziri mkuu, yamesemwa mengi juu yake. Hata safu hii ilihusika kujadili suala lake kwa mapana na marefu. Hatua yake ya kujiunga na Chadema itaibua mjadala mzito. Naona ni wajibu wangu pia kuweka bayana mambo kadhaa ili mjadala huu uweze kunoga na kueleweka. Mambo mawili yanakuja mawazoni mwangu kwa haraka.

Kwanza, zamu ya CCM kumsema Lowassa imekwisha. Kwa wakati huu, ni zamu ya Lowassa kusema na kusikilizwa. Watanzania wanataka kumpa nafasi Lowassa awaeleze na wamsikilize kama walivyoisikiliza CCM kwa miaka minane ikimsema Lowassa. Ikimtuhumu kuwa fisadi, mla rushwa na mambo mengine ya kudhalilisha.

Wakati wote huo, Lowassa alikaa kimya akiwasikiliza na wao wakatumia uhuru wao kumsema Lowassa ni nani mbele ya umma.

Kwa uhuru ule ule, ni wakati wake kusema na kusikilizwa. Anaweza kuutumia uhuru huo kusema yeye ni nani? Anaweza kutumia fursa hiyo ya kusikilizwa, kusema CCM ikoje? Anaweza pia kutumia muda wake kusema Tanzania yetu inahitaji nini? Nasisitiza tena, ni wakati wa Lowassa kusema na kusikilizwa, si wakati wa CCM kusema. Walikuwa na miaka minane kufanya hivyo na walisikilizwa sana. Hii ni zamu yake.

Pili, katika siasa, hakuna jambo linalotokea kwa bahati mbaya au kwa ajali. Mambo yote katika siasa hutokea kwa mipango ya wazi au kwa mipango ya matukio. Nina maana kuwa, kama mambo hayakupangwa kwa wazi, basi huwa yanapangwa na matukio, yaani tukio moja huandaa njia ya kutokea tukio jingine.

Ni kwa sababu hiyo napingana na wanasiasa hasa wa chama tawala wanaopenda kukejeli vyama vingine kuwa ni vyama vya matukio au vya msimu. Matamshi yao hayo yanaonyesha jinsi wasivyojua kuwa katika siasa hakuna tukio la bahati mbaya au la ajali.

Waumini wa falsafa hii ndio waliamua na kuhakikisha kuwa miundombinu ya utawala, izungukwe na idara za kijasusi na za usalama zenye weredi wa kuhakikisha hakuna matukio ya bahati mbaya katika siasa.

Kuondoka kwa Lowassa ndani ya CCM kulitabiriwa zamani na kuanza kuandaliwa. Si Kikwete wetu wala mtangulizi wake wanahusika moja kwa moja kuandaa tukio hili, bali wao walikuwa ni watekelezaji wa tukio hili. Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema kuwa upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM.

Akaongeza kuwa, watu wakikosa mabadiliko ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM. Katika kilele cha baba wa taifa kutaka kuachana na CCM, alitamka kuwa “CCM si mama yangu” na kisha akasisitiza kuwa kwake chama ni sera. Chama kikiacha sera anazoziamini, na yeye anaachana nacho.

Kilichotokea baada ya matamshi haya, ni watawala kupuuza licha ya kwamba walikuwa wanafurahia utamu wa maneno ya hayati baba wa taifa. Kwa kupuuza kwao matamshi hayo, walikuwa wanaadaa mpango mahsusi wa kisiasa ambao yawezekana ndio huu tunaoushuhudia hivi sasa. Tukio hili si ajali, bali ni mpango kabambe ulioandaliwa na wapuuzi wachache bila kujua kuwa wanatekeleza falsafa niliyoitaja.

Watanzania wameshuhudia CCM ikiacha misingi aliyoiweka hayati Baba wa taifa. Wazee wema wakalalama mpaka wakachoka. Watanzania wakashuhudia miiko ya uongozi ikipuuzwa na uongozi ukigeuzwa bidhaa sokoni.

Katika hili, hata Mkuu wa nchi alikuwa anachangishwa na watia nia ili waende kuhonga kupata kura. Pamoja na matumizi makubwa ya fedha, bado chama kikaasisi utaratibu wa fitna, majungu, na mikakati ya wizi wa kura ndani na nje ya chama kama utaratibu rasmi wa kushinda uchaguzi.

Mambo haya yalipokuwa yanatumika dhidi ya wapinzani, hakuna aliyeshtuka, lakini yalipoanza kutumika ndani ya CCM yenyewe ndipo tulipoanza kuona nuru ya kudai mabadiliko. Tulishuhudia wazee wenye heshima kama John Malecela, Salim Ahmed Salim, Fredrick Sumaye, Philip Mangula, Joseph Warioba na wengine wakidhalilishwa vibaya wakati wa chaguzi za ndani za chama hicho.

Hatuwezi kuwasahau watu kama Dk. Mohammed Ghalib Bilal, Salmin Amour; na sasa Mizengo Pinda wakidhalilishwa na mbinu zile zile za fitna wakati wa uchaguzi. Haya yote yalikuwa ni maandalizi ya kuthibitisha kuwa katika siasa hakuna tukio la bahati mbaya wala la ajali. Yote hupangwa na kutekelezwa ama kwa mipango ya wazi au kwa mipango ya kipuuzi.

Mengi yatasemwa kuhusu Edward Lowassa. Na CCM watakuwa msitari wa mbele kusema mengi. Hii haitakuwa haki kwa CCM wala kwa Lowassa. Kwangu mimi, unaoitwa uchafu wa Lowassa ni matokeo ya mfumo uliolelewa na CCM na sasa kina Lowassa ni wahanga wa mfumo walioulea wao bila kujua.

Kwa maneno mengine, Lowassa ni muasi wa mfumo alioulea ukakua kisha ukamgeuka. Waswahili husema “akuanzaye mmalize.” Kwa hiyo, mfumo alioshiriki kuulea Lowassa umetumika kumnyanyasa na yeye akaamua kuuasi.

Hili ni tendo jema lakini linalohitaji ujasiri kama wa Lowassa. Si wengi wanaweza kuuasi mfumo uliowalea. Tumeshuhudia watu wengi wakibaki wamebweteka ndani ya mfumo kandamizi bila kuchukua hatua kwa kisingizo cha uzalendo. Ukandamizaji hauna uzalendo kamwe.

Siyasemi haya kuonyesha kuwa Lowassa atashinda na hatimaye kupata kile CCM wanachodai anakimbilia kukipata kupitia upinzani. Hata kama hatafanikiwa, Lowassa ameweka rekodi ya pekee katika kizazi hiki, kwa kuamua “kufa amesimama kuliko kuishi amepiga magoti” ndani ya CCM.

Kwa viongozi wa CCM ambao wamenuna na wanaanza kusema maneno mabaya dhidi ya Lowassa, nawafananisha na mme aliyemwacha mkewe akidhani atapata shida, kisha alipogundua kuwa hajapata shida akaanza vitimbi na kugeuza shingo kama feni kila mkewe wa zamani anapopita. CCM iliamua kupitia vikao vyake kuwa Lowassa hafai. Leo kaamua kutafuta jukwaa jingine. CCM waachane naye maana ni mbaya!

Mwandishi wa makala hii ni Kondo Tutindaga, mail: tutikondo@yahoo.com

error: Content is protected !!