August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM: Ukawa ni imara zaidi yetu

Spread the love
HATIMAYE Mkutano wa Umoja wa Wanawake (UWT) kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) umikiria kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekomaa, anaandika Dany Tibason.
Samia Suluhu Hasani, Makamu wa Rais wa Serikali inayoundwa na CCM amesema, upinzani una nguvu kubwa nchini na wabunge wa upinzani wamekomaa zaidi ya wa CCM.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa ufunguzi mkutano wa UWT unaofanyika mjini humo katika ukumbi wa mikutano wa CCM Makao Makuu.
Akifungua mkutano huo Samia amesema, kwa miaka 20 upinzani umezalisha wabunge waliopevuka sana na kwamba, ni lazima umoja huo ujiuliza, je wao wanawafundisha nini wabunge wapya wa viti maalum ambao wapo bungeni mpaka wanakomaa?
Amesema, wakati wa uchaguzi mkuu, CCM imefanya kazi kubwa ili kuhakikisha inarudi madarakani kutokana na kukumbana na ugumu wa kisiasa kwa kuwa, siasa za upinzania zilikuwa na nguvu kubwa.
Mbali na hilo amesema, serikali kwa sasa inatakiwa kujiuliza, ni kwa namna gani itawakomboa akina mama ambao wapo katika mazingira magumu wakikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama huku wakitembea umbali mrefu kufuata maji.
Katika ufunguzi huo amesema, jukumu kubwa ambalo umoja huo wanatakiwa kulifanya ni kuhakikisha wanapambana na nguvu kubwa ya upinzani inayoonekana kuwa tishio.
Alisema ni wajibu wa kila mwanamke kuhakikisha anazalisha wanachama wengi na kukisemea vyema chama chake.
Samia amesema, umoja huo unatakiwa kufanya tathimini juu ya utekelezaji wa kazi zake ikiwa ni pamoja na kuona ni jinsi gani ya utoaji wa elimu kwa wabunge hususani wapya wa viti maalum katika kutekeleza hoja zao.
“Je wabunge wa Viti Maalum ambao ni wapya mnawafundisha nini wanapokuwa bungeni wakitekeleza majukumu yao? Je, waendelee kujibu na kupiga vijembe au waweze kujenga hoja na kupenyeza bungeni matakwa na mahitaji ya wanawake wenzao?” alihoji.
Pamoja na mambo mengine Samia amesema, atamshauri bosi wake (Rais John Magufuli) kuhakikisha wakati wa uteuzi wa Wakuu wa Wilaya, nafasi nyingi zinachukuliwa na akina mama.
Sofia Simba, Mwenyekiti wa UWT amesema, ili kuonesha jinsi akina mama wanavyothaminika ndani ya chama, ni vyena rais akateua Wakuu wa Wilaya wanawake wengi kwa kuwa, akina mama hao walikibeba chama wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
 “Tunakuomba mama yetu (Makamu wa Rais) uweze kumshauri rais wakati wa uteuzi wa Wakuu wa Wilaya wanawake wawe wengi kwani wanawake wengi wanaziweza hizo kazi za chini.
“Kumbuka wapo wanawake wengi wamegombea wameshindwa na wamekitumikia chama hivyo jamani wasisahulike. Je, kweli si kweli?” alihohi Simba huku akina mama wakimuitikia ‘kweliiii’.
Kwenye mkutano huo Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma amewashangaa wabunge na madiwani kwa kushindwa kuisimamia serikali na kuikosoa pale inapokosea.
Kimbisa amesema, inashangaza kuona wakati wa kampeini ya Uchaguzi Mkuu wagombea walikuwa wakijinadi kuwapelekea maendeleo wananchi, lakini baada ya kupata madaraka wamekuwa wakimya na sasa hawajihusishi na shida za wananchi wao tena.
“Kama wakati wa kampeni tulikuwa kunafanya kampeni nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba, kitanda kwa kitanda na shuka kwa shuka, inakuwaje leo hatuwezi kupeleka maendeleo kwa wananchi kwa kutumia mkakati ambao tulikuwa tukiutumia wakati wa kuomba kura?
“Haiwezekani mbunge au diwani ukashindwa kuisimamia serikali au kuikosoa pale unapoona inakosea katika mambo fulami ni wajibu wetu kuisimamia serikali” amesema Alhaji Kimbisa.
error: Content is protected !!