August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM Mwanza wamuweka mtegoni Magufuli

Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza kimemtaka Rais John Magufuli kuwatimua kazi Marry Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, kwa kukaidi maagizo ya chama hicho wakati wa kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga, anaandika Moses Mseti.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Magufuli aagize wakuu wa Wilaya za Nyamagana na Ilemela jijini hapa kusitisha zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara hao katika maeneo ya katikati ya Jiji.

Rais Magufuli aliagiza machinga kuendelea na shughuli zao katikati ya Jiji mpaka pale uongozi wa jiji hilo utakapotenga maeneo ambayo ni rafiki, huku akidai wanaweza kufunga barabara moja ili machinga hao wafanye biashara zao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mustapha Banigwa, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Nyamagana, amesema kuwa kabla ya zoezi la kuwaondoa machinga hao, Oktoba 25 mwaka huu Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ilikutana na kuzuia mpango wa Mkuu huyo wa Wilaya.

Banigwa aliyazungumza hayo kwa niaba ya chama hicho, mkoa wa Mwanza, huku akidai kuwa pamoja na kamati hiyo ya siasa kumshinikiza DC Mary Tesha kuacha utaratibu wa kuwaondoa machinga lakini alikaidi na kuendelea kusimamia uamuzi wake.

“Kitendo cha DC na Mkurugenzi wa Jiji kukaidi maagizo ya chama kinadhihirisha dharau na kiburi. Tunamuomba Rais Magufuli atengua teuzi zao na kuteua watu wenye uwezo wa kuwatumika Wananchi.

DC na DED wanafanya mambo bila kulishirikisha Baraza la Madiwani na hata Meya wa Jiji tulipomuuliza anasema suala hilo hawakushirikishwa,” amesema Banigwa.

Aidha Banigwa ameeleza hofu ya chama hicho kupoteza majimbo ya Nyamagana na Ilemela ikiwa wateule hao wa rais hawataondolewa.

“Rais aangalie maslahi mapana ya wananchi wa Mwanza, akiacha hawa watu waendelee na kazi kwenye wilaya zetu, tutakuwa tunaelekea kupoteza majimbo. DC na DED lazima pia warejeshe fedha Sh. milioni 180 zilizotumika katika zoezi la kuwaondoa machinga katikati ya Jiji,” amesema.

Hussein Kimu, mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Nyamagana, amesema maamuzi yaliochukuliwa na viongozi hao, yamekifedhehesha chama hicho na wao kama vijana katika wilaya hiyo walipinga zoezi hilo lakini walishangaa kuona machinga wakiondolewa katikati ya Jiji.

error: Content is protected !!