January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM Morogoro yaja juu

Spread the love

DOROTH Mwamsiku, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Morogoro ameoneshwa kutoridhishwa na namna migogoro ya wafugaji na wakulima inavyoshughulikiwa, anaandika Christina Raphael.

Mwamsiku amesema hayo leo wakati akitoa maazimio ya kikao cha Halmashauri ya CCM ya Mkoa yaliyoazimiwa katika kikao chao cha kawaida kilichofanyika hivi karibuni.

Amesema, haoni utendaji makini wa watendaji wa serikali wanavyoshughulikia migogoro hiyo na kuitaka serikali, vyombo vya usimamizi na utekelezaji wa sheria kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu bila kupendelea upande wowote.

Mwamsiku amesema kuwa, baadhi ya watendaji wa serikali na viongozi wanadaiwa kugeuza migogoro hiyo kuwa miradi ya kujipatia kipato huku wakionekana kukimbilia maeneo yenye matatizo mara wafugaji wanapokumbwa na matatizo huku wakiacha kufika pale wakulima wanapokumbwa na matatizo.

Amesema kuwa, CCM imesikitishwa na utaratibu wa viongozi kukimbilia maeneo yenye matatizo wakati yakishatokea badala ya kuchukua hatua kuzuia matatizo yasitokee mapema.

Hata hivyo CCM imetoa tamko la kutoingiza mifugo mipya katika Mkoa wa Morogoro kufuatia mkoa huo kwa sasa kutokuwa na uwezo wa kupokea mifugo mipya .

Pia ameiomba serikali ya mkoa kutoa tangazo la kupiga marufuku uhamiaji wa mifugo kutoka mikoa mingine.

Mwamsiku amesema, serikali ngazi ya mkoa ichukue hatua madhubuti wakilenga kuwaondoa wafugaji wavamizi kwenye vijiji vyote vya Mkoa wa Morogoro pamoja na kuwazuia wengine kutohamia.

Hata hivyo ameiomba serikali kufanya kazi ya ufuatiliaji wa kina wa malalamiko ya wakulima dhidi ya baadhi ya watendaji katika serikali na vyombo vya usimamizi wa sheria wanaoendekeza kushirikiana na wafugaji wakorofi kudhulumu au kuchelewesha utekelezaji wa madai ya fidia kwa wakulima pale wanapoharibiwa mazao yao.

error: Content is protected !!