June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM mnahofia nini – Maalim Seif

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad, mwanasiasa anayepigania haki ya kuongoza Zanzibar baada ya kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi wa Oktoba 25, amesema hakuna sababu ya viongozi wa CCM kumhofia. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

“Kwani wanaogopa nini wakati nimeshasema mimi katika uongozi wangu sitalipiza kisasi kwa mtu yeyote. Sina muda wa kushughulika na mtu katika wakati ambao ninajukumu la kushughulikia maendeleo ya wananchi,” ameema.

Maalim Seif ambaye kura za vituoni zilizoridhiwa na mawakala wa vyama vyote pamoja na maofisa wasimamizi wa uchaguzi majimboni, zinemuonesha kuwa alishinda uchaguzi, ametoa kauli hiyo alipohutubia wajumbe wa mkutano mkuu na kamati tendaji za wilaya za CUF kisiwani Pemba.

Alikwenda Pemba jana kukamilisha jukumu la kuwaeleza viongozi waandamizi wa CUF hatima ya mkwamo wa uchaguzi, ikiwa ni wiki mbili tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi wote Zanzibar.

Alifanya mkutano kama huo juzi Jumatatu kwa wajumbe na viongozi wa mikoa mitatu ya Unguja, kwenye ukumbi wa Majid, Mombasa, mjini hapa.

Amesema hakuna sababu ya viongozi wa CCM kupata hofu ya kuongozwa na Maalim Seif kwa sababu ameshapewa ridhaa na wananchi wenye mamlaka ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.

“Mimi ndiye rais niliyechaguliwa, ndiye ninayeangalia serikali nitakayoiongoza itakuaje, tena nimeshasema tutaendeleza serikali ya umoja wa kitaifa na kwa sababu vyama vyetu vimepata viti sawa vya uwakilishi, tutatoa mawaziri kwa idadi sawa,” amesema.

Amemsihi Dk. Ali Mohamed Shein akubali matokeo ya uchaguzi yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi kama alivyokubali yeye katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Amesema kwa busara kabisa, “Dk. Shein awe muungwana kwa kuridhia maamuzi ya wananchi waliopiga kura Oktoba 25 na kunichagua niwe kiongozi wao… yeye amemaliza muda wake kikatiba tangu Novemba 2, asifanye kinyongo.”

Salamu hizo alizitoa kwa viongozi wa Unguja ambako alisikika akitamba kuwa haba wasiwasi kuwa ndiye rais mpya na anachosubiri ni “kuitwa kwa ajili ya kuapishwa na kushika nafasi mara moja.”

“Nanyi msiwe na wasiwasi wowote. Mimi ndiye rais wenu mpya na tayari nimeanza kutengeneza serikali nitakayoiongoza ambayo itaendelea kuwa ya mfumo wa umoja wa kitaifa kwa kuchanganya mawaziri kutoka chama chetu CUF na wenzetu CCM, tutakuwa na mawaziri sawa kwa sawa,” amesema.

Katika serikali iliyomaliza muda wake kufuatia uchaguzi wa mwezi uliopita, Serikali iliyoundwa na Dk. Shein ilikuwa na mawaziri saba wa kila upande wa vyama hivyo vya CCM na CUF.

Katika uchaguzi wa safari hii, kila chama kimepata viti 27, CUF ikivuna viti vyote 18 vya kisiwani Pemba kwenye ngome yake isiyoshindika, na CCM ikipata viti vyake Unguja.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi tangu 1995, CUF imeongeza viti Unguja kufikia tisa. Katika uchaguzi wa nyuma, ilifikisha viti vitano.

CCM mbali na kutopata kiti chochote cha uwakilishi na ubunge Pemba, imekosa hata diwani mmoja katika wadi zote kisiwani humo. Katika uchaguzi wa 2010, ilipata madiwani wawili huko.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, chama kinachoshindwa uchaguzi kwa kupata zaidi ya asilimia tano ya kura, kitatoa jina la kiongozi atakayeteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais.

Safari hii, na kama Tume itamtangaza Maalim Seif aliyepata kura nyingi, kuwa ndiye mshindi wa wadhifa wa urais, CUF itatoa makamu wa pili, ambaye atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali kwenye Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

CUF iliteuliwa viongozi wake kuongoza wizara ya Habari; Miundombinu na Mawasiliano; Katiba na Sheria; Afya na Ustawi wa Jamii; Kilimo na Uvuvi na Biashara, Viwanda na Masoko na waziri wan chi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa rais.

error: Content is protected !!