June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM Mbarali wamsifu JK

Baadhi ya wakazi wa Mbalali, wakiwasikiliza polisi wakati walipokuwa na mgogoro wa ardhi

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali, mkoa wa Mbeya, kimempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kushughulikia mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka mitano baina ya wanavijiji 21 waliotakiwa kuhama kupisha Hifadhi. Anaandika Mwandishi wetu, Mbeya … (endelea).

Kwa mujibu wa CCM, Rais Kikwete amesikia kilio cha muda mrefu cha wananchi wilayani humo. Hatua hiyo, inakuja baada ya Aprili mwaka huu, serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kusitisha mpango wa kuvihamisha vijiji 21 vilivyokuwa vimeingizwa kinyemela kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Badala yake serikali iliagiza wananchi waendelee kuishi hapo na kuagiza kufanyiwa marekebisho ya mipaka.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali, Mathayo Mwangomo, aliwaeleza waandishi wa habari katika ofisi za CCM mkoa kuwa, serikali iliomba ardhi kwa wananchi wilayani humo kwa ajili ya Hifadhi ya Ruaha, na wananchi kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi na kulinda rasilimali walikubali.

“Wananchi licha ya kukubali kupisha kwenye ardhi ikiwa ni pmoja na kukubali viwango vya fidia, japo kwa wengine havikuwa vikilingana na gharama halisi za maisha, lakini ukafanyika ujanja na kutaka kuwahamisha,” alisema.

Mwangomo ameongeza kuwa katika mchakato wa upimaji kwa makusudi, watalaamu waliopewa kazi ya kusimamia suala hilo walizidisha mpaka na kuingia kwenye maeneo ya wananchi ambayo awali hakukuwepo makubaliano ya kuyachukua.
Amesema eneo hilo lenye vijiji 21 vilivyopo kata za Luhanga, Utengule Usangu, Mwatenga, Madibira, Imalilo Songwe, Rujewa, Igava, Miyombeni, Mapogoro na Mawindi, linatumiwa kwa makazi ya wananchi.

Wilaya hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 16,000 huku kilometa 10,000 zikiwa ni eneo l6 hifadhi.
Amesema CCM wilayani humo iliwasilisha malalamiko hayo kwa Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana wakati alipofanya ziara na aliahidi kuwa atahakikisha analifikisha suala hilo serikalini kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Mwangomo, serikali ya Rais Kikwete, inawajali wananchi wake na ipo kwa ajili ya kuwatetea na kuzipatia ufumbuzi kero zinazowakabili, hivyo kupitia waziri Nyalandu, iliagiza wananchi waachwe waendelee na maisha kwenye vijiji hivyo bila kuhamishwa.
Amesema Nyalandu pia aliagiza wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wilaya na mkoa wa Mbeya kukutana kwa ajili ya kuangalia upya mpaka uliowekwa ili kuwezesha kufanyia marekebisho GN namba 28.

“Uamuzi huu wa Nyalandu ulipokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wilayani Mbarali. Huu ni uamuzi wa kiongozi makini na mwenye kujali maisha ya watu wake,” alisema Mwangomo.

error: Content is protected !!