January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM kuwatumia Mrema, Cheyo kunadi Katiba mpya

Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema

Spread the love

MKAKATI wa siri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), “kulazimisha” kura ya maoni ya “Ndiyo” kwa Katiba Inayopendekezwa umevuja. Wanaandika Edson Kamukara na Deusdedit Kahangwa…(endelea).

Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iko shakani kukamilisha kwa wakati uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters’ Registration (BVR).

Kura ya maoni imepangwa ifanyike Aprili 30 mwaka huu; ambapo CCM tayari imeunda kamati mbili za kitaifa na jimbo ili kufanikisha mkakati huo.

Kamati hizo zitawashirikisha makundi ya watu anuai, vyama vya siasa, Asasi zisizo za kiserikali; na wanaoitwa “wadau na wakereketwa wa Katiba Inayopendekezwa” japo wenyewe hawana taarifa hiyo.

MwanaHALISIOnline limeuona waraka huo ambao washirikwa wake kutoka upinzani ni Augustino Mrema na Hussein Juma (TLP),  John Cheyo na Juma Khamis Faki (UDP), Hamad Rashid na Khadija Abdalla Ahmed (ADC).

Wengine ni Rashid Yusuph Mchenga (AFP), Mwanamrisho Ahmeed (Demokrasia Makini), Tatu Mbarouk na Peter Kuga Mziray (APPT Maendeleo), Mwanaid O. Tahir (NRA) na Juma Ali Khatib (TADEA).

Humo wameingizwa pia wasania kupitia Shirikisho lao, na wahusika ni Simon Mwakifwamba, Jacob Stephen (JB), Nasib Abdoul (Diamond), Ali Kiba, Steve Nyerere, Mrisho Mpoto, Mohamed Lyasi, Mariam Hamdan,  Hamis Mwinjuma (Mwana FA) na Mohamed Mavala.

Zinahusishwa pia Asasi sisizokuwa za kiserikali ambapo Magdalena Rwebangira atawakilisha Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Siti Abbas Ali na Salama Aboud Talib watawakilisha Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA).

Amon Mpanju na Frederick Msigala watawakilisha Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA); Shaban Muyombo, Agatha Senyagwa, Suzy Laizer, Dk Maselle Maziku, Hadija Kondo, Reuben Mtango watashawishi kwa Shirikisho la Vyama vya Wakulima Tanzania (TASO).

Mkakati huo vile vile unahusisha Mtandao wa Vikundi Vidogo vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) ambapo wapo Veronica Sophu na Catherine Sibuti; wakati William Olenasha, Makeresia Pawa, Mashavu Yahya, Said Abdalla Bakari watatoka Pastoralists Indigenous NonGovernmental Organization.

Kwa upande wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)/TAMWA mhusika ni Valeri Msoka, huku Dk. Ave-Maria Semakafu atawakilisha ULINGO; Idrissa Mustapha na Fatma Musa Juma watatoka Youth Centre, MYDO za Zanzibar.

Waraka huo unawataja pia Mary Daffa wa Tanzania NGO’s (TANGO);  Kingunge Ngombale Mwiru (Taasisi ya Tiba ya Jadi); Elizabeth Minde (KIWAKUKI) na Godfrey Simbeye Taasisi ya Sekta binafsi.

CCM wanasema kuwa katika kuhakikisha wananchi wanaipigia kura ya “Ndiyo” Katiba Inayopendekezwa, ni muhimu muundo wa Kamati ya kura ya maoni uwe na kamati ya kitaifa yenye wajumbe 300.

Katika kamati hii, kila mkoa utapangiwa wajumbe 12 ambao watakuwa na jukumu la jumla la kusimamia kampeni ya “Ndiyo” katika mkoa husika. Kwa upande mwingine CCM wanataka kamati ya jimbo iwe na wajumbe 50.

Wajumbe hao 12 wa kila mkoa watatokana na viongozi wa CCM mkoa husika ambao ni:- Mwenyekiti na Katibu wa mkoa, Katibu wa Siasa na Uenezi, Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwenyekiti wa UWT, Mwenyekiti wa Wazazi na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa, huku wajumbe wengine watano watatokana na orodha ya wajumbe 125 walioorodheshwa.

Kamati hiyo ya kitaifa, wajumbe wake wataongozwa na Philip Mangula (Mwenyekiti), Abdulrahman Kinana, Mizengo Pinda, Balozi Seif Iddi, Nape Nnauye, Mohamed Seif Khatib, Zakia Meghji,Mwigulu Nchemba, Abdallah Bulembo, Sophia Simba na Jerry Slaa.

Wengine ni Adam Kimbisa, Khadija Aboud, Emmanuel Nchimbi, Samia Suluhu Hussein, Makame Mbarawa, Anna Tibaijuka, Shamsi Vuai Nahodha, Pindi Chana, Hussein Mwinyi, William Lukuvi, Maua Daftari na Steven Wasira.

Wajumbe wengine ni Jenista Mhagama, Asha Bakari, Amina Makilagi, Eva Kihwele, Salama Aboud, Sadifa Hamis Juma, Sixtus Mapunda, Anna Abdallah, Shaka Hami Shaka, Mfaume Ali Kizigo, Wilson Mukama, Martine Shigela na Anthony Mavunde.

MwanaHALISIOnline limebaini kwamba wengi wa watu wanaoitwa “wadau na mashabiki wa Katiba inayopendekezwa,” ni wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la 201 na baadhi ya wabunge pamoja na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana.

MwanaHALISIOnline limezungumza na Dk. Bana ambaye amesema, “Hiyo ni habari mpya kwangu. Hata hivyo mimi ni mtaalam mshauri wa vyama vyote na wagombea wakiwemo. Kwa hiyo itabidi nifuatilie kujua CCM wanataka niwasaidie vipi.”

Alipotakiwa aseme kama ataipigia kura ya “Ndiyo” Katiba Inayopendekezwa, Dk. Bana amekiri na kusema, “Katiba ya nchi sio msahafu. Haiwezi kukubaliwa na watu wote kwa kila kifungu.

Agustine Mrema, alipoulizwa utayari wake wa kushirikishwa na CCM katika kamati yao, amesema “Sijapewa barua ya uteuzi. Lakini nikiletewa nitakubali.

“Huo ndio msimamo wangu tangu Dodoma tulipokuwa Bunge Maalum la Katiba. Msimamo huu unatokana na uzoefu wangu kama Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa kawaida, na Kamisaa wa Dawati la Siasa ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa kwa muda mrefu”.

Simon Mwakifamba, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Wasanii nchini, hakuwa tayari kusema kama atashiriki katika kamati hiyo akisema, “Bado mapema kuongelea jambo hilo. Sina taarifa zozote kuhusu jambo hilo. Muda ukifika nitaongea”.

Msanii maarufu, Steve Nyerere ameieleza MwanaHALISIOnline kuwa yuko tayari kuwa mjumbe katika kamati hiyo lakini akaweka bayana kwamba bila malipo hatafanya kazi hiyo.

error: Content is protected !!