SAMIA Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, amesema atashirikiana na viongozi wa chama hicho, kupitia upya sera na miongozo ya chama hicho, ili iendane na wakati. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Ametoa ahadi hiyo leo Ijumaa tarehe 30 Aprili 2021, baada ya kupitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho, kushika wadhifa huo ulioachwa na Hayati Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021.
Mkutano huo maalum wa CCM umefanyika jijini Dodoma, ambapo wajumbe wake 1862 waliohudhuria, walimchagua Samia kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa asilimia 100.
Akizungumza katika mkutano huo, Samia amesema sera na miongozo inayoelekeza itikadi, muelekeo na majukumu ya CCM, zitapitiwa ili kuangalia zinazofaa.

“Nitajielekeza kuhamasisha viongozi wenzangu katika nagzi zote, tupitie kwa kina sera na miongozo inayoelekeza itikadi, imani, muelekeo na majukumu ya chama tuone yale yanayotufaa kwa hali na mwenendo wa dunia, kwa wakati tulio nao kwa lengo la kusonga mbele,” amesema Samia.
Mwenyekiti huyo wa CCM amesema “kazi ya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi kitaendelea, nitasimamia maadili, kanuni na taratibu za chama ili kujenga chama chenye nidhamu na chenye wanachama wanaotambua wajibu wao kwa chama na Taifa lao.”
Samia amesema katika kipindi cha uenyekiti wake ndani ya CCM, ataimarisha mifumo ya chaguzi za ndani na nje ya chama hicho.
“Tutahakikisha tunaendelea na mfumo thabiti ulio wazi na kutoa haki katika michakato ya chaguzi zetu za ndani na zile za kupata wawakilishi katika dola,” amesema Samia.
Mwanasiasa huyo amesema katika kipindi cha uongozi wake ndani ya CCM, atahakikisha anarudisha imani ya Watanzania kwa chama hicho.

“katika kipindi cha uenyekiti wangu, nitashirikiana nanyi wote kuhakikisha tunasimamia misingi ya chama chetu lakini pia keundeleza utamaduni wa kujitahimini, kujisahihisha na kufanya mabadiliko kwa lengo la kuimarisha chama chetu, kujenga imani kwa wananchi sambamba na kwenda na mabadiliko yanayotokea duniani.”
Licha ya hayo, Samia ameahidi kutoa mafunzo kwa makada wa CCM ili wawe na siasa zenye tija nakistaarabu badala ya kuwa na siasa zenye kuligawa Taifa.
“Kwa kuwa chama chetu ni mzazi wa vyama vya siasa, tutaongeza wigo wa mafunzo kwa makada wetu ili waweze kukijenga chama ndani na nje kwa umma, waweze kujipanga katika kushiriki vyema siasa zenye tija na zenye kuaisisi maendeleeo endelevu kwenye Taifa letu,” amesema Samia.

Mwanamama huyo amesema “kuahamsisha siasa za kistaarabu zenye kujenga umoja wa kitaifa badala ya kujigawa kwenye makundi yanayoleta mfarakano na kukihujumu chama chetu.”
Sambamba na hayo, Samia ameahidi kuboresha masilahi ya watumishi wa CCM pamoja na kuondoa malimbikizo ya madai yao.
“Nafahamu kuna maslahi duni ya watumishi wa chama, na vilevile nafahamu kuwa kuna malimbikizo ya madai ya stahiki zikiwemo za uhamisho, malimbikizo ya madai ya stahiki za uhamisho na kustaafu, pamoja na hizo kuna changamoto ambazo ufumbuzi wake ni kukaa kama chama tujitahimini ili kuimarsiha itikadi na imani yetu,” amesema Samia.
Leave a comment