KAIMU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rodrick Mpogolo, amesema aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Hayati Dk. John Magufuli, amekiwezesha chama hicho kujitegemea kiuchumi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Mpogolo amesema hayo leo Ijumaa tarehe 30 Aprili 2021, katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, uliofanyika jijini Dodoma wa kuchagua mrithi wa Dk. Magufuli, aliyefariki dunia mkoani Dar es Salaam, tarehe 17 Machi mwaka huu.

Jana tarehe 29 Aprili 2021, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), ilimpitisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha Dk. Magufuli.
Akizungumza katika mkutano huo, Mpogolo amesema, Dk. Magufuli enzi za uhai wake, alijitoa katika kuleta mageuzi ya kimuundo na kiuchumi, yaliyokiwezesha chama hicho kujitegemea kiuchumi.
“Dk. Magufuli alileta mageuzi makubwa ndani ya chama hiki, kimuundo na kiuchumi na chama kimeweza kuimarika kiuchumi, hali iliyopelekea sasa kujitegemea. Tunaweza kusema Hayati Magufuli ameacha CCM imara na serikali madhubuti,” amesema Mpogolo.
Mbali na kuimarisha CCM, Mpogolo amesema Dk. Magufuli atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha utendaji wa Serikali pamoja na kuifikisha nchi katika Uchumi wa kati kabla ya 2025.
“Dk. Magufuli alijitoa muhanga katika kupigania maendeleo ya uchumi kwa nchi yake na kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati kabla yawaka 2025 kama ilivyokuwaimepangwa,” amesema Mpogolo.
Leave a comment