January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM ipo taabani Kilwa – Bwege

Spread the love

MTETEZI wa kiti cha ubunge, jimbo la Kilwa Kusini, Suleiman Bungara “Bwege” anasema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina hali mbaya katika jimbo hilo na hakuna namna yoyote ya kukiokoa na anguko la mara ya pili katika uchaguzi mkuu. Anaandika Charles William … (endelea).

Bungara aliyeingia kwa kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, akimuangusha kada kigogo wa CCM, Ramadhan Madabida, anasema siri ya mafanikio hayo ni maendeleo aliyowapatia wananchi jimboni.

Ameiambia MwanaHALISI Online kwamba “Huku Kilwa kusini kila kitu kimekaa sawa, nimefanya kazi kwa miaka mitano na kila mtu ameshuhudia nilivyokuwa nikipambana ndani na nje ya bunge kupigania maslahi ya watu wa Kilwa na Lindi kiujumla.”

Amesema kwamba anachofanya sasa ni kukumbushia yale aliyoyafanya pamoja na kueleza atakavyoshughulikia yaliyobakia katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Bungara anayefahamika zaidi kwa jina la utani la Bwege, amesema tangu ameanza kampeni zake, wananchi wanampokea vizuri kila anapofika kuomba kura na wameonesha kuridhika na jitihada zake.

Bungara anakabiliana na ushindani wa Hasanain Gulamabas Dewji kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye Bwege anasema hamhofii kwa kuwa, “CCM ipo taabani sana huku kwa sasa, wananchi wa Kilwa hawapo tayari kurudi tena utumwani, walishaamka na hawataki kurudi katika usingizi mzito utakaowachelewesha kufanya shughuli za maendeleo.”

Bwege anaungwa mkono na vyama vinne vikiwemo NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD) ambavyo vimeshirikiana na Chadema na CUF kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Anasema ameshafanya kampeni katika Kata zote 10 za jimbo na kuzunguka vijiji vyote 38; sasa akiwa ameanza duru la pili la kuzunguka ili kuongeza morali wa umma kumchagua tena.

error: Content is protected !!