July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM inatikiswa Z’bar

Spread the love

MSIMAMO wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoshiriki uchaguzi uliovurugwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado unatikisa, anaandika Faki Sosi.

Taarifa ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba, yapo makundi mawili ambayo kwa sasa yamekuwa mwiba; moja likiamini kurudiwa kwa uchaguzi huo na lingine likionesha hofu kutokana na msimamo wa CUF.

Hata hivyo, makada wa chama hicho wanaonesha hasara na hofu endapo mtikisiko wa kisiasa uliopo sasa utaendelea kupuuzwa na Serikali ya CCM.

“Tunakwenda lakini tuna hofu kubwa,” amezungumza mmoja wa makada aliyeomba kuhifadhiwa jina lake kutokana na nafasi yake ndani ya chama hicho na kuongeza “sijui kama tutavuka salama.”

Mohammed Yusuf Mshamba, aliyekuwa miongoni mwa wasaka kuteuliwa kugombea urais ndani ya CCM mwaka 2010 visiwani Zanzibar ameonesha mashaka kutokana na hali ilivyo sasa visiwani humo.

Akizungumza na mtandao huu leo Mshamba amesema,marudio ya uchaguzi yanaweza kuhatarisha amani kwa kuwa hakuna makubaliano kati ya vyama vikuu visiwani humo.

Na kwamba, idadi kubwa ya Wazanzibari hawako radhi kuona nchi hiyo inaingia kwenye uchaguzi mwingine mbali na ule wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

“Uchaguzi wa awali ulifutwa kinyume na katiba na kuitishwa kinyume na katiba,” amesema na kuongeza “Mwenyekiti wa ZEC,  Jecha Salim Jecha hakuwa na ushahidi wa kutosha wa kufuta uchaguzi huo.”

Mshamba amesema kuwa, uchaguzi uliofutwa umelisababisha taifa kuingia kwenye matatizo ya kikatiba na kwamba, Jecha hakuwa na sababu za msingi za kufuta uchaguzi huo.

Akikumbusha uchaguzi wa mwaka 2000 amesema kuwa, ulikuwa unahitilafu za wazi ambapo majimbo takribani 16 yalirudiwa uchaguzi lakini haukufutwa uchaguzi wote.

“Nimeshangazwa na uhalali wa matokeo ya Rais wa Jamhuri yaliyotokana na uchaguzi huo amabao ulikuwa chini ya uangalizi mmoja na uharamu wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wawakilishi, na Madiwani.

“Tumepiga kura tano mwaka jana 25 Oktoba ya Rais wa Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Wawakili na Madiwani (Masheha), iweje matokea ya kwenye uchuguzi uleule mengine yawe halali na matokeo mengine yasiwe halali? Alihoji Mshamba.

Mshamba amesema, yeye anaamini kwenye mazungumzo ingawa wakuu wa vyama vya siasa vilivyokinzana kwenye uchaguzi marudio ya uchaguzi walikutana takribani mara nane lakini mazungumzo yaligonga mwamba.

Hata hivyo amesema, mgombea urais ambaye amesimamishwa au kufukuzwa uwanachama na chama chake, hapaswi kuwa mgombea wa nafasi yeyote kwa mujibu wa katiba pia hana haki ya kupewa ulinzi.

“Huwezi kuwa mgombea bila kuwa mwanachama wa chama chochote, hii haiwezekani lakini unapoona mambo haya yanalazimishwa mwenye akili timamu atajua nini kinatafutwa hapo.”

Juma Said Makame Mkazi wa Donge ameuambia mtandao huu kwamba, kilichofanywa na ZEC ni sawa na mtu mkubwa kujifanya mtoto.

“Mfano wa uchaguzi uliofutwa ni sawa na mtu kuwa na sufuria la wali, halafu unatoa wali wa juu kwamba ni msafu lakini wa chini una kinyesi.

“Hivi ukiambia wa chini ulikuwa na kinyesi na huu wa juu hauna, je unaweza kula chakula hicho? Yaani inakuwaje matokeo yaliyohusu bunge na urais bara yawe sahihi na yaliyohusu Zanzibar yawe haramu?” ameshoji.

Kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar tarehe 28 Oktoba mwaka jana kumeibua sintofahamu na hata kufikiriwa kuibuka kwa vurugu pale uchaguzi huo utapolazimishwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.

error: Content is protected !!